Unapokutana na Doreen Moraa Moracha, ni vigumu kutovutiwa na tabasamu yake. Ni vigumu kufikiria kwamba unayekutana naye ni binti ambaye amepitia mengi maishani, zaidi kutokana na hali yake ya kiafya.
Mara ya kwanza kwake kufahamu kwamba alikuwa anaishi na Virusi Vinavyosababisha Ukimwi (VVU) ilikuwa "bahati" alipokuwa na umri wa miaka 13.
Alimsikia daktari akimwuliza mamake, ambaye alimjibu daktari kwamba walifahamu alikuwa na virusi tangu alipokuwa na miaka minane. Miaka mitano awali.
Wazazi wake walishangazwa sana na taarifa hizo walipofahamishwa kuhusu hali yake mara ya kwanza na hawakuzikubali.
"Wakati huo ufahamu wa jinsi mama anaweza kumwambukiza mtoto wake akiwa tumboni au wakati wa kunyonyesha ulikuwa mdogo sana. Walifikiria nilikuwa nimerogwa na walianza kumtembelea mganga ambaye alifanya matambiko.
"Nilipokosa kupata nafuu, walimtafuta kasisi ambaye alinibatiza wakisubiri nife."
Anakumbuka wakati huo alikuwa na kaka mdogo wa miaka mitatu ambaye alikuwa ananyonyeshwa na mamake.
Aliugua na kufariki muda mfupi baadaye.
Mamake alikuwa ndiye mwenye virusi lakini babake hakuwa na virusi hivyo. Ndugu zake wengine hawana virusi hivyo.
Doreen hakuamini aliyoyasikia mara ya kwanza wazazi wake waliokuwa wanazungumza na madaktari kuhusu hali yake..
"Nilijua watu walio na Ukimwi huugua na kufariki. Tena, watu huambukizwa Ukimwi kupitia kushiriki ngono. Haiwezekani," anasema.
Tangu walipogundua alikuwa ana virusi, wazazi wake walikuwa wakimpa dawa za kumuongezea nguvu mwilini.
"Mwaka uliofuata, mamangu aliugua sana. Mimi pia nilianza kuugua. Alipopata afueni kidogo, alinipeleka hospitalini."
Ni wakati huo, mwaka wa 2005, ambapo Doreen alijulishwa rasmi kwamba alikuwa ana virusi, lakini akatulizwa moyo na kuambiwa: 'Siku moja, utapata nafuu.'
Alipewa dawa za kupunguza makali ya VVU, maarufu kama ARVs.
Hakupokea habari hizo kama habari za kuhuzunisha, ingawa alitahadharishwa kwamba aweke habari hizo zikiwa siri.
Ingawa jamaa zake wa karibu walifahamu ukweli kuhusu hali yake, aliiweka siri hadi mwongo mmoja baadaye.
Alipokaribia kumaliza masomo chuoni, alipewa nafasi kama mkurufunzi katika kitengo cha Tume ya Kuajiri Walimu Kenya (TSC) ambacho kiliangazia kuwahamasisha walimu na wafanyakazi wengine kujali afya yao.
"Tulikuwa tunawashauri watu wapimwe kubaini iwapo wana VVU kwa hiari. Tulikuwa na sehemu ya watu kupimwa. Lakini wengi walikuwa wanaikwepa sehemu hiyo."
"Tuliporejea afisini, nilimwambia bosi wangu kwamba labda watu hawakufahamu vyema umuhimu wa kupimwa ndio maana walikuwa wanakwepa."
Mkubwa wake kazini alifahamu hali yake, na ndipo akatoa wazo la Doreen kujitokeza kutangaza hali yake.
"Sikupokea pendekezo hilo vyema. Itakuwaje, niwafichulie watu wengine, watu tusiofahamiana hata kidogo hali yangu? Baada ya muda, niliamua kuandika simulizi yangu ambayo, mwenyewe baada ya kuisoma ilinigusa sana. Kisha, nilimwandikia mhariri wa masuala ya afya katika gazeti moja kuhusu hali yangu kupitia barua pepe. Mhariri huyo baadaye aliniita kwa mahojiano."
Ni hapo ambapo hatimaye mwezi Mei mwaka 2015, kisa chake kilitangazwa hadharani, kupitia makala iliyochapishwa gazetini ikiwa na jina ana anwani yake, na ikiwa na kichwa 'Kwamba nina Ukimwi hakujafuta ndoto zangu'.
Watu waliposoma kumhusu, alitumiwa ujumbe si haba, na wengine wakamwandikia kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Baadhi waliomfahamu walishangaa na kumwuliza mbona akaweka hali yake kuwa siri muda mrefu hivyo.
"Niliifunga kwa muda akaunti yangu ya Facebook siku hiyo," anasema.
Siku iliyofuata hata hivyo, aliifungua tena akaunti yake na 'kuendelea na maisha'.
Alianza pia kutafutwa na vyombo vingine vya habari vilivyovutiwa na maisha yake ambapo miongoni mwa mengine alihojiwa kwenye runinga.
Aligundua kwamba watu wengi walitaka kufahamu zaidi kumhusu.
Ni hapo ambapo wazo la kutumia mitandao ya kijamii lilimjia.
Kujifunza kukubali hali yangu'
"Vijana wengi wanatumia Facebook na mitandao mingine ya kijamii. Nilijua kwamba ningewafikia watu wengi zaidi kupitia jukwaa hilo. Nilijua ningebadilisha maisha ya mtu fulani pahali kupitia njia hiyo," anasema.
"Siku zilivyoendelea kusonga, nimejifunza kukubali hali yangu na kuishi nayo."
Mwaka 2016, kwa pamoja na wengine walio na VVU, walianzisha kundi la Hope Alive, ambapo walisaidiana kwa kutiana moyo na kupokezana ushauri.
Anaeleza kundi hilo kama "pahali salama kwa watu kuzungumza na kufungua nyoyo zao. Tungekumbushana, kwa mfano kwamba wakati umefika wa kunywa ARV. Palikuwa pahala pa faragha."
"Watu wengi walianza kujihisi kwamba 'hatuko peke katika hili'. Tupo wengi ambao tunaishi na VVU," anasema.
Baadaye alijiunga na shirika kwa jina Blast ambalo ni la kuwahamasisha watu kuhusu Ukimwi. Shirika hilo hutembelea shule mbalimbali kuwahamasisha wanafunzi na vijana katika juhudi za kupunguza viwango vya maambukizi mapya ya VVU.
Shirika hilo hupewa kazi na serikali kupitia Shirika la Mpango wa Taifa wa Kukabiliana na Ukimwi na Magonjwa ya Zinaa (Nascop).
Usichokifahamu hakiwezi kukudhuru?
"Watu huwa na dhana kwamba 'kile nisichokijua mimi hakiwezi kunidhuru'. Ukimwi pia huhusishwa na mapenzi ya kiholela na kutokuwa mwaminifu katika ndoa au uhusiano."
"Unapopimwa na kujua hali yako, iwapo hauna virusi, unaishi salama na kuchukua hatua za kujikinga. Ukifahamu kwamba umeambukizwa, unayapanga vyema maisha yako. Unajifunza kuishi na virusi vyake na kukubali hali yako."
Ni kwa nini si watu wengi hujitokeza hadharani? Mtu yeyote anaweza?
Doreen anaamini kwamba ingawa watu walioambukizwa wakijitokeza kwa wingi hilo litapunguza unyanyapaa, ni vyema kujiandaa kabla ya kufichua hali yako.
"Iwapo hauwezi kuwafichulia hata marafiki zako, utawezaje kuufichulia umma? Umma wakati mwingine huwa katili. Anza kwanza kwa kuwafichulia jamaa na marafiki zako. Kwa watakavyozipokea taarifa hizo, unaweza kujiandaa kuwafichulia wengine zaidi."
Kwa Doreen, maisha katika familia yake yalikuwa pia mchanganyiko. Wakati mwingine, baadhi ya ndugu zake walimwonea wivu kutokana na uangalizi wa karibu na "upendo" alioupokea kutoka kwa wazazi wake.
Lakini baadhi walimkubali alivyokuwa na hata walikuwa wanamkumbusha wakati ukifika wa kunywa ARVs.
Ukiwa na virusi vya Ukimwi si lazima ukondeane
"Kuwa na VVU hakuna maana kwamba utakondeana, kuwa na upara kichwani na kuonekana kudhoofika kimwili.
"Siku hizi kutokana na ARVs pamoja na watu kuanza matibabu mapema, unaweza kuishi maisha yenye afya.
"Kulikuwa na picha hiyo ya mtu aliyekonda sana, anayeugua na aliyedhoofika sana kiafya kama nembo ya Ukimwi, hali si hiyo tena."
Kunao wale ambao wamekuwa wakimtamani na hata kumuandikia ujumbe wa kuomba urafiki kwenye mitandao ya kijamii kila wakiona picha zake.
Doreen anasema: "Nimeanza kuzoea hilo."
Kikombe cha Babu wa Loliondo
Muda baada yake kugundua kwamba alikuwa ana virusi vya Ukimwi, Doreen alitazama taarifa za 'kutia moyo' kwenye runinga.
Zilikuwa ni taarifa za mamia ya watu waliokuwa wanasafiri hadi Loliondo nchini Tanzania kupokea tiba ya kipekee, kikombe kimoja tu, kutoka kwa mzee ambaye alifahamika sana kama Babu wa Loliondo.
Wengi wa walioshirikishwa walisimulia jinsi tiba hiyo ilivyowaponya.
Ni kutokana na hilo ambapo Doreen alimshawishi mamake wafunge safari hadi Loliondo.
"Nilikuwa na matumaini kwamba tungepona. Babu alikuwa anawaambia watu kwamba si yeye mwenye kuponya, na si kikombe chake, bali ni imani uliyo nayo. Tulikuwa na imani ya kutosha, tungekosaje imani?," anasema.
Safari ya kwenda iliwachukua siku moja unusu na kurudi siku moja, na kikombe wakalipia Sh100.
Aliporejea Kenya, kwa imani kwamba tiba ya Babu ingemponya, aliacha kunywa ARVs.
Lakini hatua hivyo ilimwathiri sana na akadhoofika kiafya, hadi kulazimika kurejea hospitalini.
Anawashauri wengine kutovutiwa na waganga au wahubiri wanaoahidi tiba.
"Kufikia sasa, hakuna tiba yoyote. Ni hatua tu zinazopigwa katika kutafuta tiba. Usiache kunywa ARVs."
No comments:
Post a Comment