Nyumba hizo ni zile ambazo zimejengwa mita 91 kutoka Barabara ya Morogoro, ikiwa ni mwendelezo wa awamu ya pili ya ubomoaji wa zaidi ya nyumba 1,000 zilizokuwa ndani ya hifadhi hiyo ya barabara hiyo. Tayari nyumba zilizokuwa ndani ya mita 121.5 kati ya Kimara na Kiluvya zimeshabomolewa.
Novemba 20, Tanroads ilitoa notisi ya siku 30 kwa wananchi wanaomiliki nyumba hizo kuzibomoa au kuondoka kabla haijaanza kuzibomoa.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, meneja wa Tanroads wa mkoa, Julius Ndyamkama alisema hawataki kuwaumiza wananchi wao wakati wa sikukuu kwa kuwa ni kipindi cha kupunguza dhambi kwa Mwenyezi Mungu.
“Hatuna mpango wa kuwafanya wananchi wasifurahie sikukuu yao. Hiki ni kipindi cha maajilio bwana. Tunataka tupunguze dhambi kwa Mwenyezi Mungu,” alisema.
Meneja huyo alisema licha ya kuwa wametoa notisi kwa wananchi mpaka Desemba 20, haimaanishi watawavunjia nyumba zao kwa kuwa hata wao wana huruma.
Juzi, Mwananchi iliambiwa na baadhi ya wananchi hao kuwa inawawia vigumu kuhama na kumudu mahitaji mengine ya siku kuu, gharama za usafirishaji mali zao, kodi, ada na maandalizi ya msimu mpya wa masomo na kuomba mamlaka ziwaonee huruma.
“Hapa nawaza kipato ninachopata, watoto wanatakiwa ada mwezi Januari, wanataka nguo za sikukuu, huko niendako nahitaji kupanga chumba. Kwa hiyo ni majukumu juu ya majukumu,” alisema mkazi wa Kimara Bucha, Anastazia Alfred.
Ubomoaji wa nyumba ambazo ziko ndani ya hifadhi ya barabara hiyo umedumu kwa takribani miezi sita tangu Juni. Ubomoaji huo pia uligusa nyumba 32 za ibada, vituo sita vya mafuta na vinne vya afya.
Pia, walibomoa nyumba kadhaa za vigogo wa Serikali na wanasiasa akiwamo mbunge wa Mikumi, Joseph Haule ‘Profesa J’.
No comments:
Post a Comment