Sunday, December 3

Uhaba wa fedha wakwamisha utafiti


Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (Muhas), kinakabiliwa na uhaba wa fedha unaosababisha kishindwe kufanya tafiti za kutosha.
Ukata huo umesababisha kupungua kwa idadi ya machapisho ya tafiti kutoka 576 kwa mwaka 2015/16  hadi kufikia machapisho 439 kwa mwaka 2016/17 sawa na upungufu wa asilimia 31.8.
Kaimu Makamu wa chuo hicho, Profesa Appolinary Kamuhabwa alisema hayo jana Jumamosi Desemba 2,2017 katika mahafali ya 11 ya Muhas yaliyofanyika chuoni na kuhudhuriwa na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi ambaye ni mkuu wa chuo hicho.
Profesa Kamuhabwa amesema upungufu huo umetokana na hali ngumu ya fedha chuoni na mabadiliko ya uchumi kwa mashirika ya nje yanayofadhili tafiti.
“Tafiti zimekuwa na mchango mkubwa katika kupata ufumbuzi wa matatizo ya afya yanayoisumbua jamii ya Watanzania. Tunaiomba Serikali iendelee kuunga mkono na kuchangia katika shughuli hizi,” amesema Profesa Kamuhabwa.
Amesema kwa kipindi kirefu chuo hicho kimekuwa kikitegemea zaidi udhamini wa Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa wanafunzi wa ngazi ya uzamili.
Profesa Kamuhabwa amesema kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita ufadhili wa wanafunzi hao wanaochaguliwa kujiunga Muhas umepungua na kusababisha idadi ya wanaosajiliwa baada ya kuchaguliwa kupungua kwa kukosa ufadhili.
“Hata wale wanafunzi waliopata ufadhili kwa mwaka wa masomo 2016/17 karo zao bado hazijalipwa hadi sasa hali inayosababisha uendeshaji wa mafunzo kuwa mgumu,” amesema.
Amesema Muhas inaendelea kufanya jitihada za kuwasiliana na wadau wa ndani na nje ya nchi ili kuongeza upatikanaji wa udhamini kwa wanafunzi wa uzamili na uzamivu.
 Katika mahafali hayo, wanafunzi 1,024  wamehitimu masomo yao kwa ngazi mbalimbali.

No comments:

Post a Comment