Leo ni siku ya Ukimwi Duniani. Kila mwaka, Dunia huadhimisha siku ya Ukimwi Disemba 1 ikiwa ni wakati wa kukumbuka wale waliokufa kutokana na maradhi hayo.
Wachambuzi wa masuala ya kiafya wanasema kuwa pia ni wakati ambao hutumika kuonyesha juhudi na azma ya mataifa kuwasaidia wale wanaoishi na virusi vya HIV, kufanya kazi kwa pamoja kuzuia kuenea kwake na hatimaye kumaliza maambukizo.
Matamko kutoka nchi mbalimbali yanasema siku ya Ukimwi Duniani pia ni wakati wa kusheherekea na kuwashukuru watafiti, wahudumu, familia, marafiki na jamii ambao wanafanya kazi kwa pamoja kutokomeza changamoto kubwa.
Kwa upande wake Serikali ya Marekani imesema kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR) siyo kwamba imeokoa na kuboresha maisha ya mamilioni ya watu, lakini pia imetengeneza mpango wa dunia katika kukabiliana na HIV/AIDS.
Balozi wa Marekani nchini Ethiopia Michael Raynor amesema Takwimu za hivi karibuni za PEPFAR zinaonyesha kuwa dunia inapiga hatua katika kudhibiti maradhi ya HIV/AIDS.
Hili linaonekana katika nchi ambazo bado zinaelemewa na mzigo mkubwa wa kukabiliana na maradhi haya—kitu ambacho kilikuwa kinaonekana ni vigumu kudhibiti siyo muda mrefu uliopita. Lakini pamoja na mafanikio hayo huu siyo wakati wa kujibweteka.
Balozi huyo amesema kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson wakati wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa 2017, alizindua Mkakati wa PEPFAR mpya kwa ajili ya kusukuma udhibiti wa HIV/AIDS (2017-2020).
“Mkakati huo unaonyesha ushujaa na nia na msimamo wetu thabiti juu yale tunayotaka kuyafikia. Inathibitisha kuwa serikali ya Marekani, kupitia PEPFAR, itaendelea kusaidia juhudi za kudhibiti maambukizi ya ukimwi katika nchi zaidi ya 50."
Pia ni kuhakikisha wanapata huduma za tiba ya Ukimwi kwa wanajamii wote wakiwemo makundi yaliyo hatarini kutokana na maambukizo, amesema Michael Raynor.
Ameongeza kuwa huko Ethiopia, PEPFAR imewekeza takriban Dola bilioni 2 kusaidia kukabiliana na HIV/AIDS.
“Hivi leo juhudi zetu zimewezesha kuwapatia dawa za kurefusha maisha ya waathirika wa ukimwi kwa Waethopia 433,909, wakiwemo watoto," amesema.
Taarifa ya PEPFAR inaonyesha kuwa taasisi hiyo imeweza kuwezesha wanawake wajawazito takriban milioni moja nchini Ethiopia kupima ukimwi na kupata ushauri nasaha na pia imehakikisha kuwa zaidi ya watoto mayatima 280,000 na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na wale wanaowalea wanapata uangalizi na msaada wa huduma muhimu wanazohitaji.
No comments:
Post a Comment