Kumekuwa na mzozo wa muda mrefu kuhusu udhibiti wa mji wa Jerusalem kati ya Waisraeli na Wapalestina.
Mji huo kwa sasa huwa umegawanywa mara mbili, Jerusalem Mashariki na Jerusalem Magharibi.
Jerusalem ya Magharibi hutazamwa na Israel kama mji wake mkuu nayo Jerusalem Mashariki hutazamwa kuwa mji mkuu wa taifa la Wapalestina (litakapoundwa), ingawa eneo hilo bado kwa kiwango kikubwa limetawaliwa na Israel tangu vita vya 1967.
Tangu wakati wa vita hivyo, Israel imejengwa nyumba za walowezi wa Kiyahudi takriban 200,000 ambao huishi Jerusalem Mashariki, hatua iliyoshutumiwa na jamii ya kimataifa. Eneo hilo huishi Wapalestina takriban 370,000.
Israel ilitangaza 1980 Jerusalem yote kuwa mji wake mkuu wa milele, lakini nchi nyingi duniani hazikubali azimio hilo.
Hivyo basi, balozi za nchi za kigeni katika Israel ziko nje ya Jerusalem, katika mji wa Tel Aviv.
Mzozo huo umefufuliwa tena kutokana na hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani kutarajiwa kuutambua mji huo kama mji mkuu wa Israel.
Mataifa mengi ya Kiarabu yameshutumu hatua hiyo ya Bw Trump na kusema itazidisha uhasama Mashariki ya Kati.
Lakini ni kwa nini mji huu huzozaniwa hivyo? Mwandishi wa BBC Erica Chernofsky anachambua.
Dini tatu
Mji huu huwa na umuhimu mkubwa kwa dini tatu kuu - Ukristo, Uislamu na Uyahudi. Dini zote tatu humuangazia Abraham anayetajwa kwenye Biblia na Koran kama mmoja wa waanzilishi au mababu wa imani.
Ni mji ambao umedhibitiwa na dini hizo kwa vipindi mbalimbali katika historia.
Kwa Kiebrania, mji wa Jerusalem hufahamika kama Yerushalayim na kwa Kiarabu al-Quds. Kwa Kiswahili, jina lake halisi ni Yerusalemu. Mji huo ni miongoni mwa miji ya kale zaidi ambayo ipo hadi sasa duniani.
Ni mji ambao umetekwa, ukabomolewa na kuharibiwa na kisha kujengwa tena.
Kila sehemu ya ardhi yake ukichimba kwenda chini hufichua enzi fulani katika historia yake.
Ingawa umekuwa chanzo cha ubishi na mzozano kati ya dini mbalimbali, dini zote huungana kwa pamoja kuungama kwamba ni eneo takatifu.
Ndani yake kuna Mji Mkongwe, ambao una njia nyembamba, vichochoro na nyumba za kale. Kuna maeneo manne makuu na kila eneo, majengo huwa tofauti. Kuna eneo la Wakristo, Waislamu, Wayahudi na Waarmenia. Eneo hilo huzungukwa na ukuta mkubwa wa mawe. Hapo, kunapatikana baadhi ya maeneo yanayoaminika kuwa matakatifu zaidi duniani.
Kila eneo kati ya maeneo hayo manne (unaweza kuyaita mitaa) huishi watu wa aina moja. Wakristo wana maeneo mawili, kwa sababu Waarmenia pia ni Wakristo. Eneo lililotengewa Waarmenia, ambalo ndilo ndogo zaidi kati ya hao manne, lina vituo vya kale zaidi vya Waarmenia duniani.
Jamii ya Waarmenia imehifadhi utamaduni wake wa kipekee ndani ya Kanisa la St James na nyumba kubwa ya utawala. Maeneo hayo mawili yamechukua sehemu kubwa ya mtaa huo wa Waarmenia.
Kanisa
Ndani ya mtaa wa Wakristo, kuna Kanisa Kuu la Kaburi na Ufufuo wa Yesu Kristo, ambalo ni muhimu sana kwa Wakristo kote duniani.
Hupatikana katika eneo ambalo lina umuhimu mkubwa katika kisa cha kusulubiwa, kufariki na kufufuka kwa Yesu.
Kwa mujibu wa utamaduni wa Kikristo, Yesu alisulubiwa hapo, katika Golgotha, au mlima wa Calvary. Kaburi lake linapatikana ndani ya kanisa hilo la kaburi na inaaminika kwamba hapo ndipo alipofufuka.
Kanisa hilo husimamiwa kwa pamoja na madhehebu mbalimbali ya Kikristo.
Sana huwa ni wahudumu wa kanisa la Kiothodoksi la Ugiriki, watawawa na mapadri wa Francisca kutoka Kanisa Katoliki la Roma na wengine kutoka kanisa la Waarmenia.
Kuna pia wahuudmu kutoka kanisa la Waothodoksi kutoka Ethiopia, Coptic na Syria.
Ni eneo ambalo mamilioni ya mahujaji wa Kikristo husafiri kila mwaka kwenda kuliona kaburi wazi la Yesu na kutafuta ufunuo na kuomba katika eneo hilo.
Msikiti
Mtaa wa Waislamu ndio mkubwa zaidi kati ya maeneo hayo manne na ndani yake kunapatikana madhabahu ya Dome of Rock (Kuba ya Mwamba) na Msikiti wa al-Aqsa kwenye eneo linalofahamika na Waislamu kama Haram al-Sharif, au Mahali/Hekalu Patakatifu.
Msikiti huo ndio eneo la tatu kwa utakatifu katika dini ya Kiislamu na husimamiwa na wakfu wa Kiislamu ambao hufahamika kwa Kiarabu kama Waqf.
Waislamu huamini kwamba Mtume Muhammad alisafiri kutoka hapo hadi Mecca usiku na aliomba pamoja na roho za manabii wengine wote. Hatua chache kutoka hapo kunapatikana Dome of the Rock (Kuba ya Mwamba) ambapo kuna jiwe la msingi. Waislamu huamini kwamba ni kutoka hapo ambapo Mtume Muhammad alipaa mbinguni.
Waislamu hutembelea eneo hilo takatifu kila wakati katika mwaka, lakini kila Ijumaa wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, mamia ya malelfu ya Waislamu hufika kuomba kwenye msikiti huo.
Ukuta
Katika mtaa wa Wayahudi, kunapatikana Kotel, au Ukuta wa Magharibi ambao ni masalio ya ukuta wa nje uliozunguka lililokuwa Hekalu Takatifu.
Ndani ya hetalu hilo kulikuwa na Patakatifu pa Patakatifu, eneo takatifu zaidi katika dini ya Kiyahudi.
Wayahudi huamini kwamba hapo ndipo kulikuwa na jiwe la msingi ambapo kutoka kwake dunia iliumbwa.
Kadhalika, wanaamini ni hapo ambapo Abraham alikuwa amejiandaa kumtoa kafara mwanawe Isaac. Wayahudi wengi huamini kwamba Dome of the Rock ndipo lilipokuwa eneo takatifu zaidi ndani ya hekalu lililofahamika kama Patakatifu pa Patakatifu.
Leo hii, Ukuta wa Magharibi ndilo eneo la karibu zaidi ambalo Wayahudi wanaweza kufanya maombi yao.
Husimamiwa na Rabbi wa Ukuta wa Magharibi na kila mwaka hutembelewa na mamilioni ya mahujaji.
Wayahudi kutoka kila pembe ya dunia hutembelea eneo hilo kuomba na kukumbuka utamaduni wao, hasa nyakati za siku kuu za kidini.
Ukuta huo pia hufahamika kama Ukuta wa Maombolezo.
No comments:
Post a Comment