Wednesday, December 6

Chama cha wanasheria kutofutwa


Mtwara. Naibu katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju amesema Serikali haina mpango wa kukifuta Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), badala yake itashirikiana na viongozi wa taasisi hiyo kuboresha upungufu uliopo ili kukidhi mahitaji.
Mpanju amesema hayo leo Jumatano Desemba 6,2017 wakati wa maadhimisho ya wiki ya sheria katika kanda ya kusini mkoani Mtwara yanayofanyika kwenye viwanja vya Mashujaa vilivyopo Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Amesema sheria iliyopo imepitwa na wakati kutokana na kuwepo ongezeko la mawakili, hivyo inatakiwa kufanyiwa marekebisho kukidhi mahitaji yaliyopo na kutengeneza mazingira mazuri katika tasnia hiyo.
“Serikali haina wazo la kufuta chama cha wanasheria kwa sababu ndicho chombo kinachowaunganisha na kutoa msaada wa kisheria. Tunachotaka kufanya ni kuweka mazingira mazuri kwa lengo la kuboresha ili kukidhi mahitaji,” amesema Mpanju.
Mwenyekiti wa chama cha wanasheria kanda ya kusini, Stephen Lekeya amesema walikuwa na hofu ya kufutwa TLS kwa kuwa walishapewa bango kitita kwa ajili ya kutoa maoni.
“Tulikuwa na hofu baada ya aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria kutoa kauli juu ya kufutwa kwa chama chetu si kwa maneno bali tulishapewa bango kitita kwa ajili ya kutoa maoni ya kuwepo bodi itakayosimamia chama hiki na kitakuwa chini ya Serikali,” amesema Lekeya.
Amesema katika maadhimisho hayo mwitikio wa wananchi wa kupata huduma ya msaada wa kisheria umekuwa mdogo.
Lekeya amesema wamepata idadi ndogo ya wananchi wanaohitaji huduma ya msaada wa kisheria kwa sababu ama hawaelewi dhana ya msaada wa kisheria, watu hawana matatizo ya kisheria au wameogopa kwamba watatozwa fedha kwa kuwa mawakili wapo.

No comments:

Post a Comment