Saturday, November 18

Zitto ataka Serikali kununua tumbaku ya wakulima


Urambo. Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ametaka Serikali kununua tumbaku yote ya wakulima iliyoshindikana kununuliwa.
Akihutubia wananchi leo Ijumaa katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kijiji cha Kalemela A, Kata ya Muungano wilayani Urambo Zitto ameishangaa Serikali kutumia fedha nyingi kununua ndege aina ya bombardier zinazopakia watu wachache badala ya kuwekeza kwenye kilimo kinachoajiri wananchi wengi.
Zitto amesema katika ziara yake amezunguka vijijini na kushuhudia nyuso za huzuni, huku wananchi wakimwambia tumbaku ya mwaka jana haijauzwa na msimu mpya umeanza.
“Serikali makini ingefanya nini kwenye kadhia hii ya tumbaku? Sisi ACT- Wazalendo tungekuwa madarakani tungenunua tumbaku yote ya ziada ya wakulima kwa kutumia kasma ya fedha za dharura kwenye Fungu la 50 Wizara ya Fedha,” amesema.
Amesema Serikali iliwahimiza wananchi kufanya kazi kwa bidii, lakini baada ya kuzalisha kwa wingi wanaadhibiwa kwa kukosa masoko.
Zitto ameshauri Serikali kutafuta soko kwa mfumo uliosema ni wa G to G (Government to Government) na kuuza tumbaku hiyo na kurejesha fedha hizo kwenye mfuko wa dharura.
Amesema wakati asilimia 65 ya Watanzania wanategemea kilimo kama ajira, kilimo kimekuwa kikishuka na kusababisha wakulima kuendelea kuwa masikini na kukosa chakula.
“Tunazalisha watu zaidi kuliko chakula, ni dhahiri tunaelekea kubaya,” amesema Zitto.
Amesema katika hali hiyo ya kudumaa kwa kilimo bado wakulima wa Tabora hawajafutwa machozi na zao lao la tumbaku wakati ndilo linaloingiza fedha za kigeni kuliko korosho.
“Serikali ipo tayari kutumia Sh1 trilioni kulipia ndege ambazo ni Watanzania asilimia tano wanapanda kuliko kuokoa wakulima 1.4 milioni wa tumbaku nchi nzima kwa Sh150 bilioni tu, tena ikiwa fedha hizo zinarudi ndani ya muda mfupi,” amesema Zitto.
Amewataka wananchi wa kijiji hicho kuchagua mgombea udiwani wa chama hicho ili apambane kuhakikisha tumbaku ya mwaka jana inanunuliwa.
Amesema Ilani ya Uchaguzi ya ACT -Wazalendo ilitangazwa na Taasisi ya Mviwata (Muungano wa vikundi vya wakulima) kuwa ilani bora zaidi kuhusu masuala ya kilimo kuliko ilani za vyama vyote katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kuwa ilipendekeza kuwapo kwa Hifadhi ya Jamii kwa Wakulima.

No comments:

Post a Comment