Tuesday, November 7

ZITTO ATAKA ASHITAKIWE



KIONGOZI wa Chama cha ACT- Wazalendo , Zitto Kabwe amelitaka Jeshi la Polisi limshtaki mahakamani ili madai yake dhidi ya sheria ya takwimu yapate tafasiri ya kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Kituo cha Polisi cha kushughulikia makosa ya uhalifu wa kimtandao eneo la Kamata jijini Dar es Salaam, alisema anataka kesi hiyo ipelekwe mahakamani ili tafasiri sahihi ya kisheria kuhusu masuala ya takwimu itolewe.
“Sheria ya takwimu ni miongoni mwa sheria zilizokuwa zinapigiwa kelele na wabunge kabla ya kupitishwa lakini Serikali ilifanya haraka kuipitisha huku ikiwa na upungufu katika baadhi ya vipengele. Upungufu huo unanyima uhuru wa kutoa taarifa,” alisema Zitto.
Alisema ni wakati mwafaka kwa Polisi kuifikisha kesi yake hiyo mahakamani ili mgongano uliopo uweze kupatiwa majibu ya kisheria na chombo hicho.
“Itakuwa ni kesi ya kwanza ya takwimu kufikishwa mahakamani tangu sheria hii ilipopitishwa na Bunge na hicho ndicho ninachokitaka kwa sababu kesi za takwimu haziwezi kumalizika kinyemela kwani zinaweza kuleta utatanishi,” alisema Zitto.
Awali kabla ya kuhojiwa kuhusu takwimu alizozitoa zikipingana na za serikali kuhusu ukuaji wa uchumi, Zitto alisema ACT  kilipanga kufungua kesi ya kuondoa vipengele vinavyokandamiza uhuru wa kutoa taarifa na maoni katika sheria ya takwimu.
Alisema hilo likifanakiwa litatoa tafasiri ya kisheria na kuondoa vipengele vinavyokandamiza utoaji wa taarifa.
Kabla ya kufika Kituo cha Polisi Kamata, Zitto alikwenda Kituo cha Polisi Chang’ombe kusikiliza tuhuma anazoelekezewa kuwa alitoa maneno ya uchochezi katika baadhi ya mikutano yake ya kisiasa.
Zitto aliwasili katika kituo hicho saa 10:37  na kutoka saa 4:47 baada ya kutakiwa aripoti tena Novemba 17, 2017.
Alisema polisi walimweleza faili lake bado lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hivyo arudi Novemba 17.
“Nimefika kituoni kuitikia wito wa polisi kama nilivyoambiwa wiki iliyopita lakini wamesema faili langu lipo kwa DPP ambaye analipitia kabla hajaamua kama napelekwa mahakamani au la,” alisema Zitto.
Jana viongozi wa ngazi za juu wa ACT- Wazalendo, walihojiwa na Polisi wa Kitengo cha Makosa ya Uhalifu wa Kimtandao na Takwimu kuhusu takwimu za uchumi zilizotolewa na Zitto.
Waliohojiwa ni Kaimu Mwenyekiti, Yeremiah Maganja, Katibu Mkuu, Doroth Semu na Mkurugenzi wa Ulinzi, Mohamed Babu.
Viongozi hao walifika kituoni hapo saa 3:00 na kutoka saa 9:00 alasiri.
Mwenyekiti Maganja, aliwaambia waandishi wa habari baada ya kuhojiwa kuwa lengo la mahojino hayo ni kupata ukweli wa taarifa za takwimu zilizotolewa kwenye kikao cha kamati kuu ya chama hicho.
“Kamati kuu ya chama chetu imeitwa kuhojiwa lakini unajiuliza kuwa polisi wanaweza kuiita Kamati Kuu ya CCM kuwahoji? ili ni jambo la kushangaza sana ndani ya nchi yetu,” alisema Maganja.
Alisema wakiwa katika mahojiano hayo walitakiwa kutoa majina ya wajumbe wengine wa kamati hiyo pamoja na namba zao za simu ili waweze kuitwa kuhojiwa, jambo ambalo wamelitekeleza.
“Tumewapa namba za simu pamoja na kuwaandikia majina ya wajumbe wengine wa kamati kuu ili waweze kuwaita na kuwahoji kwa sababu wanatoka mikoa tofauti,” alisema.

No comments:

Post a Comment