Tuesday, November 7

JPM AWANG’OA WAKURUGENZI WALIOSHINDWA KUJIBU SWALI LAKE

RAIS Dk. John Magufuli, ametengua uteuzi wa wakurugenzi wa Halmashauri za Manispaa ya Bukoba, Erasto Mfugale na Hamashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini, Mwantumu Dau, kwa kushindwa kueleza kuhusu fedha za Mfuko wa Barabara (Road Fund) zilizotumwa katika halmashauri zao.
Alitengua uteuzi huo jana muda mfupi baada ya kumaliza kuhutubia wananchi katika hafla ya uzinduzi wa Uwanja wa Ndege wa Bukoba.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Ikulu jana, ilisema wakurugenzi hao watapangiwa kazi nyingine.

ILIVYOKUWA
Rais Magufuli akiwa uwanjani hapo, aliwaita wakurugenzi hao na kuwataka waeleze kiasi cha fedha za Mfuko wa Barabara kilichotumwa kwa bajeti ya mwaka 2017/18 katika halmashauri zao.
Aliyeanza kuulizwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Bukoba, Mfugale ambaye alishindwa kujibu.
“Bajeti ya Manispaa ni Sh milioni 33, na kuna mapato ya ndani na ya Serikali Kuu ambayo ni pamoja na fedha za elimu bure na mishahara ambayo ni Sh bilioni 19 kwa mwaka. Fedha hizi zinakuja kwa wakati unaotakiwa,” alisema Mfugale.
Rais Magufuli aliendelea kumuuliza tena fedha za Mfuko wa Barabara ni kiasi gani, lakini mkurugenzi huyo alishindwa kujibu.
“Nani anakumbuka fedha za barabara ni kiasi gani, naweza kuteua mkurugenzi mpya leo,” alisema Rais Magufuli.
Baada ya hapo, alifuatia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini, Mwantumu, ambaye pia alijibu kwa kusema hakumbuki kiasi cha fedha kilichotolewa.
Alisema anapokea fedha nyingi za miradi mbalimbali, si rahisi kukumbuka fedha zilizotumwa na Serikali za bajeti ya mwaka huu.
“Ndiyo mimi ni mkurugenzi, nina idara nyingi sana mheshimiwa Rais, naona mweka hazina anisaidie… naogopa kusema uongo,” alisema.
Kauli hiyo, ilionekana kumkera Rais Magufuli, ambaye alisema: “Huwezi kunijibu hivyo mimi.”
Baada ya hapo, aliitwa Meya wa Manispaa ya Bukoba, Chief Karumna, aliyeokoa jahazi baada ya kueleza mchanganuo wa fedha za bajeti, ikiwamo ukarabati wa barabara na stendi kuu ya Bukoba.
“Angalau wewe umejieleza vizuri, leo nimewasamehe, siku nyingine mtaondoka. Kwenye fedha za Serikali sitanii mimi, nataka fedha hizi zitumike vizuri,” alisema Rais Magufuli.

MASILAHI YA WATUMISHI
Rais Magufuli alisema Serikali imetenga zaidi ya Sh bilioni 156 kwa watumishi wa Serikali na kuanzia mwishoni mwa mwezi huu, itaanza kulipa promosheni zote zilizokuwa zimesimama.
Pia aliagiza watumishi wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora waliohusika kuidhinisha madeni yasiyo halali kuchunguzwa na vyombo vya dola.
Alisema Serikali imeanza kupitia madai ya baadhi ya wafanyakazi na kati yake majina 110 yamekwishapitiwa ambayo wanadai zaidi ya Sh bilioni 115.2.
Rais Magufuli alisema wakati anayapitia baadhi ya majina hayo, alibaini kuwapo madai hewa ya baadhi ya watumishi, ambayo yalikwishaidhinishwa malipo yake na maofisa wa Wizara ya Utumishi na kuwasilishwa Wizara ya Fedha kwa mchakato wa malipo.
“Kuna baadhi ya majina mengine nitayataja hapa. Kuna mtu anaitwa Jackson Kaswahili Robert wa Ukerewe, yeye anadai Sh bilioni 7.626,  tulipoyapitia na kuyakagua tumebaini hadai chochote.
“Mwingine ni Mwachano Ramadhan Msingwa, huyu anatoka Bagamoyo, yeye anadai Sh bilioni 1.754, lakini kwenye ukaguzi tumekuta anadai Sh milioni 2 tu.
“Yuko pia Gideon Zakayo wa Mafia, yeye alikuwa anakaimu nafasi, anadai Sh milioni 104 za kukaimu nafasi hiyo.
“Mnaweza mkaona ni kwa jinsi gani tumekuwa na watu ambao hawana uchungu kwa nchi yao na kama tusingefanya ukaguzi hizo fedha tungewalipa.
“Watumishi waliopitisha madai haya na hawa niliowataja hapa, naagiza vyombo vya dola vianze kuwachunguza, walizoea vya bure sasa havipo na mimi nitawanyoosha mpaka wanyooke,” alisema.
Pia alisema Serikali inakusudia kupeleka bungeni muswada wa mabadiliko ya sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii ili kubaki na mifuko miwili ambayo mmoja utawahusu watumishi wa serikali na mwingine wale wa sekta binafsi.
“Sh tirioni 1.2 zimelipwa katika mifuko ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya kuwalipa wastaafu, tunakusudia kupeleka muswada wa mabadiliko ya sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii ili badala ya kuwa na utitiri wa mifuko inayoshindania wanachama, ibaki miwili tu, tunataka wakati neema inapatikana wafanyakazi halali wanufaike na haya matunda na kupata wanachostahili,” alisema.

UWANJA WA BUKOBA
Rais Magufuli, aliagiza zaidi ya Sh bilioni 9 zilizokuwa zimetengwa kulipa fidia kwa wakazi 295 wa eneo la Kajunguti ili kupisha ujenzi wa uwanja mpya wa ndege, kutumika kupanua uwanja wa Bukoba ili ndege kubwa za mizigo na abiria ziweze kutua.
“Wataalamu wa wizara tumieni mahesabu yenu uwanja upanuliwe na kufikia kilometa mbili, fedha zilizotengwa na nyingine zitakazopungua,” alisema.
Rais Magufuli, aliishukuru Benki ya Dunia (WB) kwa kutoa Dola za Marekani bilioni 57 kwa ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege vya Tabora, Kigoma na Bukoba na Sh bilioni 925 kwa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam na barabara.

UCHUMI
Alisema uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi na ndiyo maana WB imeamua kuikopesha Serikali mikopo yenye riba nafuu.
“Nitashangaa kama atatokea mtu mwingine aje kupingana na takwimu hizi, pakitokea mtu wa namna hiyo atakuwa kachanganyikiwa,” alisema.

MALISHO YA MIFUGO
Rais Magufuli alisema Tanzania si machungio ya mifugo kutoka nje ndiyo maana wameamua kukamata mifugo inayotoka nchi jirani na kuchukua hatua za kisheria.
Alisema hata ikitokea nchi jirani wakishika mifugo kutoka Tanzania, wachukue hatua za kisheria za nchi hizo.
Pia aliwataka wananchi wa Mkoa wa Kagera kuacha tabia ya kuvamia maeneo ya hifadhi, ikiwamo Hifadhi ya Pori la Burigi.
“Kuna walanguzi walipewa ranchi 54 wamekaa nazo na wanakodisha kwa wengine tu, hawajaziendeleza, nitawafukuza na kuwapatia watu wengine wanaoweza kuziendeleza,” alisema.

ATAMSHANGAA MWIJAGE
Alisema hadi sasa viwanda vipya 3,306 vimeanzishwa nchini na kusisitiza kuwa dhana ya Tanzania ya viwanda maana yake anamaanisha vijengwe nchi nzima.
“Kuna viwanda vipya 3,306, sina uhakika Kagera mna viwanda vingapi. Nitashangaa sana niwe na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji halafu kwenye mkoa anaotoka hakuna hata kiwanda.
“Leta viwanda huku nako ni Tanzania mimi sitasema umejipendelea… weka hata kiwanda cha Lubisi,” alisema.

WAZIRI WA UJENZI
Awali Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema ujenzi wa uwanja huo umegharimu Sh bilioni 31.95 na kati ya fedha hizo, zilizotolewa na Serikali ni Sh bilioni 6.35 na nyingine Sh bilioni 25 zimetolewa na Benki ya Dunia.
Alisema Serikali ilikopa WB Dola za Marekani milioni 57.5 ambazo zimefanikisha ukarabati na ujenzi wa viwanja vya Bukoba, Tabora, Kigoma na kuhamisha Shule ya Msingi Tumaini iliyokuwa jirani na uwanja wa Bukoba.
“Katika miradi yote hii, fedha za Serikali ni Dola za Marekani milioni 11.7 na fedha zingine zimetumika kufanya upembuzi yakinifu katika viwanja 11 nchini. Uwanja wa Bukoba utatumika mwaka mzima katika majira yote,” alisema Profesa Mbarawa.
Alisema pia katika bajeti ya mwaka 2017/18, wametenga fedha kufanya upembuzi yakinifu na ukarabati wa viwanja vya Iringa, Musoma na Songea na kwamba zabuni zimeshatangazwa.

No comments:

Post a Comment