Rais mpya wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ametangaza msamaha wa miezi mitatu kwa watu binafsi na kampuni mbalimbali ambazo zimeficha fedha za umma kinyume cha sheria nje ya nchi hiyo kuzisalimisha.
Kupitia taarifa, amesema kwamba serikali itawakamata na kuwafungulia mashtaka wale watakaokataa kufanya hivyo kabla ya msamaha huo kumalizika Februari.
"Vitendo kama hivi ni uhalifu wa hali ya juu wa kiuchumi dhidi ya watu wa Zimbabwe," Bw Mnangagwa amesema.
Tangu aapishwe Ijumaa wiki iliyopita, Mnangagwa ameahidi kukabiliana na rushwa.
"Fedha nyingi na mali ya umma vimefichwa nje ya nchi na watu binafsi na mashirika," amesema.
"Wale waliohusika wanahamasishwa kutumia fursa hii a miezi mitatu kurejesha fedha hizo na mali ili kuepuka uchungu na aibu ya kutembelewa na mkono mrefu wa sheria," ameongeza.
Mtangulizi wake, Robert Mugabe, aliondoka madarakani wiki iliyopita baada ya jeshi kuingilia kati.
Alikuwa ameongoza nchi hiyo kwa miaka 37 tangu uhuru.
No comments:
Post a Comment