Katika ziara iliyotangulia Rais Magufuli alitumia nafasi hiyo kuwaeleza wananchi ukweli mchungu ambao walitakiwa kuupokea bila ganzi.
Kilikuwa kipindi ambacho wananchi walikuwa wanalia na msaada baada ya kupata maafa ya tetemeko la ardhi la Septemba 2016, lakini yeye akawaeleza ukweli kuwa Serikali haiwezi kumjengea nyumba kila mmoja na kwamba sehemu ya michango iliyotolewa na wasamaria ingesaidia ujenzi wa miundombinu ya jumla kama barabara, madaraja, hospitali na shule.
Ni ukweli uliotakiwa kupokewa kama ulivyo kwamba badala yake wananchi wafanye kazi na wasibweteke kusubiri chakula cha msaada kwa kuwa tetemeko halikusomba migomba.
Lakini katika ziara ya hivi karibuni, Rais Magufuli alikuwa katika sura tofauti na kutoa maamuzi ambayo yalisahaulisha waathirika hata makali ya janga la tetemeko.
Hata hivyo, pamoja na hali hiyo, Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare alimweleza Rais Magufuli kuwa wapo waathirika wa tetemeko ambao bado wanalala nje kwa kukosa uwezo wa kurejesha makazi.
Kauli ya mbunge huyo ilitegemewa kuungwa mkono kwa makofi na vifijo na wananchi waliohudhuria uzinduzi wa kiwanja cha ndege cha Bukoba uliofanywa na Rais Magufuli, mbunge huyo alijikuta peke yake badala yake akiombwa amalize salamu zake mapema na kuwapa nafasi wengine.
Hata Rais Magufuli alipozungumza na wananchi hakujishughulisha kujibu ombi la Lwakatare.
Pengine hata Rais alijua kuwa shauku ya wananchi haikuwa kusikiliza tena habari za misaada ya tetemeko la ardhi, bali kujua ziara yake mpya itakuja na jipya gani.
Rais alitoa ufumbuzi wa kero zinazowakabili wananchi akiwa palepale jukwaani, hatua iliyoshangiliwa na kuonekana kama faraja inayofuta machungu yaliyopita.
Mambo mapya
Ziara hiyo ilitawaliwa na mambo mapya yaliyowahusu wananchi wa Kagera moja kwa moja na mengine kubeba mijadala ya kitaifa.
Aliruhusu wananchi wanaosubiri malipo ya kupisha ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Omukajunguti waendelee na kilimo kwakuwa suala hilo halitakuwepo tena.
Alisema badala yake Sh9 bilioni ambazo zingetumika kulipa fidia kwa wananchi hao wa Missenyi zitumike kuboresha zaidi kiwanja cha Bukoba.
Wakati wa ziara hiyo baadhi ya watendaji wa Serikali walipoteza nafasi zao baada ya kushindwa kujibu maswali mbele ya wananchi, hali iliyotafsiriwa kuwa ni kushindwa kumudu majukumu waliyopewa.
Ulikuwa ni wakati mwingine mgumu kwa watumishi wa halmashauri za Bukoba, Missenyi na Karagwe kwa kuwa hawakuwa na uhakika wa usafi kwenye maeneo yao endapo Rais angehitaji maelezo.
Kama si mvua kunyesha wakati Rais akiwahutubia wananchi wa Karagwe katika eneo la Kayanga, pengine kuna jambo kubwa lingetokea kama ilivyokuwa katika maeneo mengine alikopita.
Wakurugenzi kutimuliwa
Kabla ya kutenguliwa kwa kushindwa kutaja fungu la fedha la mfuko wa barabara, rungu lilimshukia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bukoba, Mwantumu Dau pale Rais Magufuli alipofika eneo la Kemondo na kusikiliza kero za wananchi.
Rais Magufuli alitoa maelekezo ya wananchi kutoendelea kutozwa ushuru katika soko, kwa kuwa Serikali ilipunguza mzigo huo kwa wananchi.
Alimuonya mkurugenzi kuwa suala la kukusanya ushuru lisijitokeze na halmashauri itafute vyanzo vingine vya mapato ambavyo havimuumizi mwananchi wa daraja la chini.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Erasto Mfugale kama ilivyokuwa kwa jirani yake, naye alijikuta matatani baada ya uteuzi wake kutenguliwa kwa kushindwa kutoa maelezo ya zilipo fedha za mfuko wa barabara.
Mkurugenzi huyu alirithi nafasi ya Kelvin Makonda ambaye mwaka mmoja uliopita uteuzi wake ulitenguliwa baada ya kutuhumiwa kufungua akaunti isiyo rasmi kwa ajili ya kukusanya fedha za waathirika wa tetemeko la ardhi.
Siku chache kabla ya uteuzi wake kutenguliwa, habari za ndani zinasema walikuwa na vikao na wakuu wa idara wakijipanga kwa ajili ya ziara ya Rais na kufanya mazoezi kwa njia ya kuulizana maswali.
Wakati mkurugenzi huyo aliposhindwa kutoa ufafanuzi wa fedha za mfuko wa barabara, mmoja wa wakuu wa idara alinyanyuka kwenda kuokoa jahazi baada ya Rais Magufuli kusema anayefahamu ajitokeze.
Hata hivyo, hakutimiza azma hiyo na badala yake ufafanuzi wa kuridhisha ulitolewa na Meya wa Manispaa hiyo, Chief Karumuna.
Mabango yayeyuka
Kumekuwa na utamaduni mpya wa wananchi kuonyesha mabango yenye ujumbe wa kero zao katika mikutano ya Rais John Magufuli, ambao umewavutia wengi.
Hata hivyo, mabango hayo hayakuonekana sana kwenye mikutano Kagera ikilinganishwa na mikoa mingine aliyopita hivi karibuni.
Hii ilitokana na baadhi ya mabango kuzuiwa wakati wa kuingia kwenye eneo la ufunguzi wa kiwanja cha ndege cha Bukoba, ingawa wachache walifanikiwa kupenyeza mabango yao kwa siri.
Hata hivyo, kulikuwapo na woga wa kunyanyua mabango hayo kutokana na baadhi yao kudhibitiwa na kuondolewa eneo la mkutano.
Hata mabango machache yaliyonyanyuliwa baada ya Rais kuwasili hayakuleta msisimko, ingawa mwanamke mmoja alipewa nafasi ya kuwasilisha kero zake.
Baadhi ya wananchi waliokosa nafasi ya kuwasilisha kero zao wakati Rais Magufuli akiwa Bukoba, walifunga safari na kumfuata kwenye mkutano wa Karagwe ambapo hata hivyo mvua iliyonyesha ilipunguza wingi wa matukio.
Miongoni mwa mabango hayo yalieleza kero ya Manispaa ya Bukoba kufyeka mazao ya wananchi kando ya mto Kanoni bila kuwapa muda wa kusubiri yakomae na kuvunwa.
Katika mkutano huo, Rais Magufuli aliwaeleza wananchi kama wapo wenye mabango yanayotaja kuondolewa kwenye vyanzo vya maji wajiondokee mapema kwa kuwa iliyofanyika ni kazi nzuri ya kulinda mazingira.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Rais ilizua mjadala kutokana na mkanganyiko wake, kwani akiwa Kyaka njiani kwenda Karagwe aliruhusu wananchi kufanya shughuli za kilimo cha mazao ya muda kando ya mito.
Katika eneo hilo, alielezwa jinsi mahindi yanavyofyekwa na maofisa wa mazingira wa Wilaya ya Missenyi wakati yeye anasisitiza wananchi wafanye kazi na hapo wananchi wakataka ufafanuzi.
Rais Magufuli alieleza kuguswa na hali hiyo na kuamua kumchangia Sh300,000 mwananchi aliyeibua kero hiyo na kuagiza waendelee na shughuli za kilimo bila kuondolewa.
Akiwa katika mkutano wa kuzindua barabara ya Kyaka-Bugene Rais Magufuli alisisitiza agizo lake alilolitoa akiwa Kyaka kuwa wananchi waachwe kuendelea na shughuli za kilimo kando ya mto maadamu shughuli hizo hazifanyiki kwenye vyanzo.
Vibali vya sukari
Katika ziara hiyo ilizuka hoja ya wananchi wa Missenyi kununua sukari kwa bei kubwa ikilinganishwa na walaji walio mbali na eneo hilo lenye Kiwanda cha sukari cha Kagera.
Akiwa eneo la Bunazi wananchi walilalamika kununua sukari kwa Sh2,800 tofauti na maeneo mengine inaponunuliwa kwa Sh2,500.
Walisema sukari ya kiwanda hicho kabla ya kuwafikia walaji wa Missenyi lazima kwanza isafirishwe hadi Mjini Bukoba (umbali wa kilometa 61) na baadaye kurudishwa ikiwa imepanda bei ili kufidia gharama za usafiri.
Kutokana na madai hayo, Rais Magufuli aliacha amemsimika wakala wa bidhaa hiyo kutoka kiwandani ili wananchi wa Missenyi wapate sukari kwa bei nafuu. Pia, Rais Magufuli aliagiza wawekezaji wa viwanda vya sukari wakutane na kujadili jinsi ya kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo ili kuziba pengo la upungufu wa tani 130,000 unaojitokeza kila mwaka.
Alisema kama watakutana na jambo hilo kuwezekana, atapiga marufuku moja kwa moja uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi.
Magufuli na Museveni
Ziara ilihitimishwa kwa kukutana na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni katika mpaka wa Mutukula ambapo walizindua kituo cha pamoja cha forodha ili shughuli zote za forodha zifanyike eneo moja.
Rais Magufuli alisema hatua hiyo pamoja na kuokoa muda kwa wasafirishaji wa bidhaa mbalimbali mpakani pia itaongeza makusanyo ya kodi kwa nchi zote mbili na kukuza uchumi.
Rais Museveni alisema hatua hiyo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa nchi hizo na kuwataka wafanyabiashara kutumia fursa zinazopatikana katika nchi hizo kwa kuwa wanapunguziwa vikwazo vilivyokuwepo.
No comments:
Post a Comment