Nimefarijika sana nilipomsikia Spika wa Bunge, Job Ndugai akiwataka wabunge wa CCM watimize wajibu wao wa kikatiba wa kuwasemea wananchi badala ya kupongeza hata pasipostahili kupongeza.
Ibara ya 63(2) ya Katiba ya Tanzania iko wazi kuwa Bunge ndicho chombo kikuu ambacho kitakuwa na madaraka kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake.
Kauli hii ya Spika, naamini imewapa faraja Watanzania walio wengi, ambao wanaona kama uchangiaji wa baadhi ya wabunge hauna tija kwa sababu unatawaliwa na dhihaka na vijembe.
Ni dhahiri Spika aliona mwelekeo usioridhisha wa baadhi ya wabunge, hawa wa chama hicho tawala ambayo haikulenga kuboresha mpango huo bali kupongeza na kujikita kwenye majimbo yao.
Lakini, bahati mbaya sana wako wabunge wanaoomba kuchangia na kutumia karibu muda wote kujibu hoja za wabunge wa upinzani, ilihali wapo mawaziri ndani ya Bunge ambao wana wajibu huo.
Labda kabla sijaingia kwa undani katika mada hii, ni vyema nikawakumbusha kile ambacho alikisema Spika, ambacho naamini kinapaswa kiende hadi kwenye Bunge la Bajeti na wakati wa kujadili miswada mbalimbali.
Ndio maana Spika akasema, “Katiba iliweka utaratibu kwamba mipango ya nchi itapita hapa (bungeni) kwanza nyinyi muijadili. Halikuwekwa hivyo kwa bahati mbaya. Liliwekwa hivyo ili nyinyi mseme kwa niaba ya wananchi.
Akaongeza, “katika mambo ya msingi kama haya fungukeni. Msijifunge funge hapo ooh mimi CCM. CCM haitaki mipango mibovu. Ni wakati wenu wa kusema tumsaidie Waziri na tuisaidie Serikali ili tusonge mbele.”
Baada ya hali hiyo, Spika akasema “Na unapoomba nafasi ya kusema hapa uwe umejiandaa. Sio ile tu naunga mkono nafanya hivi unakaa chini”.
Kwa mtizamo wangu na kwa wosia huu wa Spika Ndugai, nafikiri sasa huu ni wakati muafaka kwa wabunge bila kujali wa CCM au wa upinzani, kuisimamia Serikali pasipo hofu ya kuhojiwa katika vikao vya chama.
Wapo wabunge ambao wameusoma ujumbe wa Spika na kuuelewa na kweli “wamefunguka” kama ambavyo Spika alitarajia wote wafanye hivyo.
Lakini mimi ningependa kwa moyo huo huo, wabunge hao waisimamie Serikali ili iendeshe nchi kwa utawala bora unaoheshimu utawala wa sheria.
Sote tunafahamu tuna mihimili mitatu ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama ambayo inaoongozwa kwa kanuni kuu moja ambayo ni kutoingiliana katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku.
Bunge kazi yake ni kutunga sheria na kupitisha bajeti, Serikali ni kusimamia utekelezaji wa sheria na shughuli za kila siku za Serikali na mahakama ni kutafsiri sheria na kutoa haki.
Ukiona mhimili mmoja unajiona ni bora na kudharau mwingine kama ilivyotokea katika suala la bomoabomoa, ujue uko mgogoro wa kukosekana kwa utawala bora unaoheshimu utawala wa sheria.
Sote ni mashahidi kwamba zipo nyumba zimebomolewa kibabe licha ya kuwapo amri za mahakama, haya ni mambo ambayo Bunge linapaswa kuisimamia Serikali ili iheshimu utawala wa sheria.
Ni lazima tujitafakari kama taifa ni mbegu ya aina gani tunaipandikiza katika taifa linalojipambanua kuheshimu misingi ya utawala bora inayoheshimu utawala wa sheria na kuheshimu Katiba.
Ibara ya 3(1) ya Katiba yetu ya mwaka 1977 imeeleza wazi kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na kijamaa, yenye kufuata msukumo wa vyama vingi vya siasa ulioanza 1992.
Takwa hilo la kikatiba likaongezewa nguvu na Kanuni za Maadili vya vyama vya siasa za mwaka 2007, kama zilivyotangazwa katika gazeti la Serikali namba 2015 ya Oktoba 12 mwaka 2007.
Kifungu cha 4(1) (c), kimetaja kazi nyingine ni kujadili na kushindanisha sera zake na zile za chama kingine kikiwamo chama tawala kwa lengo la kutaka kukubalika kwa wananchi.
Leo vyama vya siasa vimezuiwa kufanya mikutano ya hadhara kwa tamko la Rais ambalo kwa ujumla wake linalalamikiwa kukiuka katiba, lakini wabunge wamekaa kimya. Hili la Ndugai liende na kuhoji hili.
No comments:
Post a Comment