Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri amejiuzulu wadhifa wake, na kuilaumu Iran kwa kuingilia masuala ya ndani ya mataifa ya Kiarabu. Alisema pia anahofia maisha yake katika mazingira ya sasa ya kisiasa nchini mwake.
Akitangaza kujiuzulu kwake ambako kumekuja kwa kushitukiza siku ya Jumamosi, Hariri alisema katika hotuba iliyotangazwa moja kwa moja kupitia televisheni, kwamba alihisi "njama dhidi ya maisha yake" katika mazingira yanayofanana na yaliokuwepo kabla ya baba yake, waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Rafik Hariri.
Rafiki Hariri aliuawa katika mripuko wa bomu pamoja na watu wengine 21 katika mji mkuu, Beirut, Februari 2005 katika mazingira ambayo mpaka leo hii hayajatolewa ufafanuzi. Saad Hariri pia ameilaumu Iran, akisema ilikuwa inaingilia masuala ya ndani ya mataifa ya Kiarabu na kuchochea machafuko.
Mwanasiasa huyo wa Kisunni mwenye umri wa miaka 47, amejiuzulu chini ya mwaka mmoja baada ya kuundwa kwa serikali yake, ambayo tawi la kisiasa la Hezbolla ni sehemu yake. "Iran inataka kuwa mwamuzi wa hatma ya mataifa ya kanda Mashariki ya Kati. Hezbolla ndiyo tawi la Iran siyo tu nchini Lebanon, lakini pai katika mataifa mengine ya Kiarabu," alisema Hariri.
"Katika miaka ya karibuni, Hezbollah imetumia nguvu ya zana zake za kivita kulaazimisha mambo," alisema akisoma hotuba ilioandaliwa. Hariri ameituhumu Iran kwa kuchochea uhasama miongoni mwa watoto wa taifa moja na kuunda taifa ndani ya taifa -- kiasi kwamba yenyewe ndiyo inao usemi wa mwisho kuhusu uendeshaji wa mambo nchini Lebabon.
Nguvu kuliko jeshi la taifa
Kundi la Hezbolla ni mshirika muhimu wa rais wa Syria Bashar al-Assad katika vita vya utawala wake dhidi ya Kundi linalojiita Dola la Kiislamu na makundi mengine ya upinzani. Linaungwa mkono na Iran na ndiyo kundi pekee la nchini Lebabon lililobakiza silaha zake baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya 1975-1990. Nguvu yake ya kijeshi imeongezeka tangu wakati huo na sasa inazidi hata ile ya vikosi vya kijeshi vya taifa.
Kundi hilo linadai ndiyo ngome pekee ya kuaminika dhidi ya nchi jirani ya Israel, na kukataa kwake kusalimisha silaha ndiyo kiini cha mgogoro wa kisiasa nchini Lebanon. Wanachama wa Hezbollah wametuhumiwa kuhusika na mauaji ya Rafiki Hariri, mtu aliekuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Lebanon baada ya vita.
Hariri alipata utajiri wake nchini Saudi Arabia, ambako mwanae Saad Hariri alizaliwa. Riyadhi ndiyo hasimu mkuu wa kikanda wa Iran, na ushindani wa ushawishi katika kanda umejitokeka katika migogoro inayoendelea nchini Iraq, Syria na Yemen.
Ofisi ya rais wa Lebanon Michel Aoun, kiongozi mkongwe wa Kikristu anaeshirikiana na Hezbollah, ilitoa taarifa ikithibitisha kwamba Hariri amekabidhi barua yake ya kujiuzulu.
Rais wa Labenon Michel Aoun anamsubiri Hariri arudi nyumbani kuzungumzia mazingira ya kujiuzulu kwake.
"Rais Aoun anasubiri Hariri arudi Beirut ili kumuuliza kuhusu mazingira yaliopelekea uamuzi wake na baadae kuamua kuhusu hatua zinazofuata," ilisema taarifa kutoka ofisi hiyo. Hariri alisema katika hotuba kwamba mazingira ya kisiasa nchini Lebanon yanafanana kabisaa na yaliokuwepo kabla ya kuuawa kwa baba yake.
Mauaji hayo ya Februari 2005 yalisababisha mabadiliko makubwa ya ghafla ya kisiasa yaliopelekea kujiondoa kwa jeshi la Syria kutoka Lebanon.
Atahri za kisiasa kwa Lebanon
Walid Jumblatt, mmoja wa wanasiasa wakubwa nchini Lebanon, na kiongozi maarufu zaidi wa Druze, alisema kujiuzulu kwa Hariri kunaweza kuiathiri vibaya nchi hiyo ambayo tayari inakabiliwa na hali ngumu.
Alihoji kwamba kujiuzulu huko ndiyo idhara ya karibuni zaidi ya mvutano kati ya Saudi Arabia na Iran, na kutoa wito wa kuzidisha juhudila kidiplomasia kutatua mgogoro huo. "Lebabnon ni nchi ndogo sana ilioko katika mazingira hatarishi kuweza kuhimili mzigo wa kisiasa unaoambatana na kujiuzulu kwa Hariri. "Nitaendelea kutoa wito wa kuwepo na mazungumzo kati ya Saudi Arabia na Iran."
No comments:
Post a Comment