Thursday, November 16

Waziri Mkuu azuiwa kujibu maswali


Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai amemzuia  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kujibu maswali mawili ya papo kwa hapo kutoka kwa wabunge kwa sababu hayakuwa maswali ya kisera.
Spika amezuia  maswali ya wabunge Susan Lyimo wa Viti Maalum (Chadema) na Mbunge wa Karagwe (CCM), Innocent Bashungwa huku akimwambia Bashungwa kuwa hata swali lake lilikuwa halieleweki.
Hayo yamejitokeza leo Alhamisi wakati Majaliwa akijibu maswali ya papo kwa hapo kutoka kwa wabunge ikiwa ni utaratibu uliowekwa na Bunge kila siku ya Alhamisi asubuhi kabla ya kipindi cha maswali na majibu.
Katika swali lake kwa Waziri Mkuu, Lyimo alihoji kumekuwa na malalamiko  kutoka kwa watumishi wa umma ambao walistahili kupandishwa madaraja Novemba mwaka jana.
“Hapa nina barua iliyotoka kwa katibu mkuu utumishi juzi tu akisema watumishi 60,000 waliokuwa wapandishwe vyeo Juni, 2016 hawatapandishwa na badala yake watapandishwa Novemba mwaka huu,”
“Kwa maoni yangu naona watumishi hawa wameonewa sababu itakuwa na athari mwaka mzima hawa watu hawataingiziwa michango inayolingana na mishahara yao,” amesisitiza Lyimo..
Hata hivyo, kabla ya hajafikia hatua ya kuulizwa swali, Spika aliingilia kati na kusema “hayo ndio maswali ninayoyakataa. Mimi nataka uulize swali la kisera moja kwa moja. Swali linasemaje?
Huku akiendelea, Lyimo alihoji ni  kwa nini Serikali inawahujumu wafanyakazi wake na mbali na kuwahujumu akitaka kujua kwa nini inawapunguzia morali na kuhoji kama itawalipa fedha hizo.
Kabla ya kujibu Spika akasema, “Napata taabu kuliruhusu hilo swali. Kwa sababu linahusu barua ambayo siyo lazima waziri mkuu ameshaiona. Tunaendelea na swali linalofuata.”
Bashungwa katika swali lake ambalo nalo lilikataliwa amesema wakulima wa kahawa wanakabiliwa na changamoto ya kukopa fedha kutoka kwa madalali, katika kipindi cha kuandaa mashamba.
Amesema wakulima hutakiwa kulipa fedha hizo kipindi cha mavuno na wakati mwingine wakati kahawa ziko shambani na kutolea mfano wa Mkoa wa Kagera kwamba tatizo hilo ni changamoto kubwa.
“Je waziri mkuu, Serikali ipo tayari kuingilia kati kwa kuweka utaratibu kupitia benki ya wakulima ili kupata mikopo ya riba nafuu? Aliuliza Bashungwa na ndipo Spika akasema maneno yafuatayo;
“Mheshimiwa Bashungwa mpaka sasa hivi nakusikiliza sijajua swali lako ni nini. Mheshimiwa Bashungwa kaa chini. Tunaendelea.”

No comments:

Post a Comment