Thursday, November 16

Kindamba azungumzia kubadilika kwa TTCL


Dar es Salaam. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Waziri Kindamba amesema mabadiliko ya sheria iliyounda kampuni hiyo na kuifanya kuwa shirika la umma kutaliimarisha shirika hilo na Serikali haitakuwa na woga wa kuweka mtaji.
Amesema sasa Serikali inamiliki kwa asilimia 100 kampuni hiyo baada ya kumlipa mbia mwenza ambaye alikuwa na hisa 35, Bharti Airtel ya India kiasi cha Sh14.7 bilioni na kujitoa katika umiliki wa kampuni hiyo ambayo ilibinafsishwa.
Akizungumzia muswada wa sheria uliopitishwa na bungeni juzi, Kindamba amesema sheria hiyo ya Shirika la Mawasiliano Tanzania italiwezesha shirika hilo kutengeneza faida ya kati ya Sh7 – 8 bilioni na kutekeleza majukumu yake mengine kwa mujibu wa sheria.
Mtendaji huyo amesema kabla ya kubinafsisha, shirika hilo lilikuwa likipeleka serikalini gawio la Sh1 bilioni lakini kwa zaidi ya miaka 15 baada ya kubinafsishwa halijawahi kupeleka gawio.  Amesisitiza kwamba mwaka huu wa 2017/18, TTCL itapeleka serikalini gawio la Sh1 bilioni.
“Miongoni  mwa mapungufu yaliyojitokeza kwenye sheria ya awali ni kuwa sheria hiyo ilililenga kuwezesha mazingira ya ubia ndani ya TTCL, hitaji ambalo sasa halipo kutokana na TTCL kurejea mikononi mwa Serikali kwa asilimia 100,”
“Kuna baadhi ya mambo ambayo tulikuwa tunayafanya lakini hayapo kwenye sheria, tulikuwa tunasaini makubaliano tu. Sasa Serikali ikaona ni bora kufanya mabadiliko ya sheria ili iendane na mahitaji,” amesema Kindamba.
Kindamba amebainisha kwamba kumekuwa na upotoshaji kwamba shirika hilo sasa linakwenda kuuawa na sheria hiyo, hata hivyo amewahakikishia wananchi kwamba sheria hiyo italiimarisha shirika hilo na kuwa litakaloongoza kwa mawasiliano nchini.
Amewahakikishia watumishi kwamba ajira zao ziko salama, madeni yote ambayo kampuni hiyo inadai na kudaiwa yatalipwa kwa kadri ya makubaliano waliyoingia na huduma zinazotolewa zitaendelea kama kawaida.
“Nimepokea simu nyingi sana za watu wakitaka kujua hatma ya kampuni hii, niwaambie tu kwamba kilichobadilika ni sheria kutoka kuwa Sheria ya Kampuni ya Simu Tanzania na kuwa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania,” amefafanua Kindamba.

No comments:

Post a Comment