Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa wajumbe wa Bodi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA), na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Mhandisi Deusdedit Kakoko, kukamilisha Skana mpya (haipo pichani), ambayo inajengwa kwa ajili ya ukaguzi wa mizigo inayoingia Bandarini hapo ambayo haijakamilika hadi sasa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amesema anasikitishwa na utendaji wa Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kutofanya maamuzi kwa wakati hali ambayo inachangia malalamiko kuongezeka Bandarini hapo. Aidha, Mbarawa amesema Serikali inapeleka Naibu Mtendaji Mkuu mpya wa shughuli za Uendeshaji Bandarini hapo kutokana na aliyekuwepo kushindwa kusimamia majukumu yake ipasavyo.
Profesa Mbarawa amesema hayo leo wakati wa ziara ya kushtukiza aliyoifanya bandarini ikiwa ni siku chache baada ya Rais John Magufuli, na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kufanya ziara ya kustukiza na kubaini madudu bandarini hapo. Ziara ya Waziri Mbarawa ni mwendelezo wa ziara mbalimbali bandarini hapo kubaini uendeshaji na utendaji wa shughuli zinazotolewa na Mamlaka hiyo.
Muonekano wa Skana mpya ambayo inajengwa kwa ajili ya ukaguzi wa mizigo inayoingia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ambayo haijakamilika hadi sasa.
“Nimelazimika leo kuwaita Watendaji na Bodi ya TPA ili kuwaeleza kasoro zenu ambapo inaonesha wazi kuwa asilimia kubwa ya mambo yanayotokea humu ni kuwa mnakuwa wazito katika kutoa maamuzi”, amesema Profesa Mbarawa. Amesema katika bandari hiyo ipo mizigo ya kahawa ambayo imefika bandarini tangu mwaka 2014 huku kukiwa hakuna sababu za kueleweka za wenye mali kutochukuwa mizigo yao.
Profesa Mbarawa amesema hahitaji wasaidizi ambao wanakaa katika vikao na kulipana posho ila wanapaswa kufanya kazi ya kuangalia shughuli zote za bandari. “Kama hamtabadilika nitaendelea kuja katika bandari hii ili kuchukua hatua pale ambapo inaonekana kwani haipendezi kila kukicha malalamiko kutokea,” amesisitiza Waziri Mbarawa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Profesa Ignatus Rubaratuka (Wakwanza kushoto), wakati akikagua shehena ya kahawa iliyohifadhiwa Bandarini hapo kwa muda mrefu.
Aidha, Waziri Mbarawa ameitka bodi na menejimenti kuhakikisha kuwa inatatua changamoto iliyopo katika bandari ya kushusha na kupakia mizigo kutoka Zanzibar na kuingia Tanzania Bara ambapo wafanyabiashara wanalalamikia utaratibu unaotumika kuwahudumia. Amesema haingii akilini kuona mizigo inayotoka au kwenda Zanzibar kutozwa kodi baada ya masaa huku inayotoka nje ya Tanzania ikitozwa baada ya siku saba.
Kuhusu ujio wa Naibu mtendaji Mkuu mpya Mbarawa aliitaka Bodi na menejimenti kumpa ushirikiano ili aweze kutoa matokeo chanya kwenye bandari. “Tunaleta Naibu Mtendaji Mkuu mpya ambaye atasimamia operesheni, naomba apewe ushirikiano ili kusaidia Serikali huyu ambaye anakaimu tunamuondoa ameshindwa kwenda na kasi yetu,” amefafanua Profesa Mbarawa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akikagua shehena ya kahawa iliyohifadhiwa tangu mwaka 2014 hadi sasa katika ghala iliyopo katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Dar es Salaam. Pembeni yake ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka hiyo, Profesa Ignatus Rubaratuka akishuhudia ukaguzi huo.
Akizungumza baada ya ziara hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya TPA Ignas Rugaratuka, amesema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa wanaitendea haki nafasi waliyopewa kwa kusimamia mabadiliko ndani ya bandari. Amesema tangu waingie wamekuwa wakipambana kuhakikisha kuwa mapungufu ya TPA yanaisha ambapo wamefanikiwa kurekebisha kwenye utawala kwa kutoa mafunzo kwa watumishi na kuzuia wizi ambao ulikuwa umekithiri.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko, amesema kuwa tangu aingie katika mamlaka hiyo wamekuwa wakifanya jitihada za kurekebisha mapungufu na kumuahidi waziri kuwa ataongeza jitihada zaidi.
“Kama ni mabadiliko tumefanya makubwa sana hasa katika utawala na uongozi ila kila anayehusika katika sekta hiyo anapaswa kutoa msaada,” amesema Mkurugenzi Mkuu.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alipofika Bandarini hapo leo wakati wa ziara ya kushtukiza kuangalia uendeshaji wa huduma Bandarini hapo.
No comments:
Post a Comment