Thursday, November 30

Mwaziri wa Uganda watebelea mgodi Tanzania


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa pili kushoto) na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Madini wa Uganda, Lokeris Peter (kushoto) wakitembelea mgodi wa Dhahabu wa Blue Reef uliopo Rwamgasa. Wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Lughumbi na kulia ni mmiliki wa mgodi huo, Christopher Kadeo.

Mawaziri Wanne kutoka Uganda wakiongozwa na mwenyeji wao Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo Agosti 29, 2017 walitembelea migodi ya dhahabu ya Mkoani Geita inayomilikiwa na Watanzania. Miongoni mwa migodi iliyotembelewa ni Mgodi wa Dhahabu wa Blue Reef uliopo Rwamgasa, Mgodi wa Dhahabu wa Busolwa Gold Mine Project uliopo Nyarugusu na Kituo cha Mfano cha Uchimbaji Madini ya Dhahabu cha Tan Discovery kilichopo Rwamgasa.

Mawaziri hao waliwasili nchini Tanzania Agosti 27, 2017 kwa ajili ya zira ya siku mbili ya kujifunza juu ya Usimamizi wa Sekta ya Madini hususan suala la Uendelezaji wa Uchimbaji Mdogo wa Madini. Kwa mujibu wa Naibu Waziri Nyongo, Mawaziri hao wametembelea migodi hiyo ili kuona namna gani migodi hiyo inaendesha shughuli zake na namna ambavyo serikali imekuwa ikiwasaidia kuhakikisha wanakuwa na uchimbaji madini wenye tija. “Wamekuja kujifunza, kuangalia Sera zetu, Sheria zetu na mchango wa Serikali katika kuwasaidia wachimbaji wadogo,” alisema.

Alisema walipendekeza kutembelea migodi inayomilikiwa na Watanzania ili kujionea namna ambavyo wazawa wanavyoendesha shughuli za uchimbaji madini ikiwa na pamoja na kuzungumza nao ili kupata uzoefu wa uendeshaji wa shughuli husika na kubaini ushirikiano uliopo baina yao na Serikali.

Akizungumza kwa niaba ya Mawaziri wa Uganda, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Madini wa Uganda, Lokeris Peter alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi Barani Afrika zilizopiga hatua kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini hususan eneo la Uchimbaji Mdogo wa Madini ikilinganishwa na nchi zingine walizotembelea.

"Uamuzi wa kufanya ziara nchini humu unafuatia uzoefu wa muda mrefu wa Tanzania kwenye masuala ya uchimbaji wa madini hususan namna ambavyo Tanzania imeweza kurasimisha suala la uchimbaji mdogo," alisema Waziri Peter.

Awali kabla ya kuwasili Mkoani Geita, ujumbe huo wa Mawaziri kutoka Uganda; Agosti 28, 2017 ulikutana na Waziri wa Madini, Angellah Kairuki ambapo ulielezwa masuala mbalimbali yanayohusu sekta husika ikiwemo Sera, Sheria na Kanuni za Madini pamoja na masuala yanayohusu Wachimbaji Wadogo wa madini.

Mawaziri kutoka Uganda waliofanya ziara hiyo ni Waziri wa Nchi- Madini, Lokeris Peter, Waziri wa Nchi- Mambo ya Ndani, Obiga Kania, Waziri wa Nchi- Mamlaka ya Mji Mkuu wa Kampala,  Namugwanya Bugembe na Waziri wa Nchi- Masuala ya Uchumi, Dkt. Kasirivu Atwooki.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) akiongozana na Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Madini nchini Uganda, Lokeris Peter (kulia kwake) mara baada ya kuwasili kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Busolwa Gold Mine Project uliopo Nyarugusu.
Mawaziri kutoka Uganda wakiwa pamoja na mwenyeji wao, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo walipotembelea mgodi wa Dhahabu wa Blue Reef uliopo Rwamgasa ili kujionea shughuli zinavyoendeshwa mgodini hapo.
Mawaziri kutoka Uganda wakimsikiliza mmiliki wa Mgodi wa Dhahabu wa Blue Reef, Christopher Kadeo (hayupo pichani) baada ya kutembelea eneo (shimo) linalochimbwa Dhahabu. Kutoka kushoto ni Waziri wa Nchi- Mambo ya Ndani, Obiga Kania, Waziri wa Nchi- Masuala ya Uchumi, Dkt. Kasirivu Atwooki, Waziri wa Nchi- Madini, Lokeris Peter na Waziri wa Nchi- Mamlaka ya Mji Mkuu wa Kampala, Namugwanya Bugembe.


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa nne kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri kutoka Uganda mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.

No comments:

Post a Comment