Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Luteni Kanali Michael Mtenjele alieleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana.
Alisema hali za majeruhi hao zinaonesha matumaini kiafya kutokana na juhudi za wataalamu za kuwapatia tiba.
Luteni Mtenjele alisema majeruhi watano baada ya kufanyiwa uchunguzi wameonekana kuwa na vipande vya bomu sehemu za mishipa na kwamba jitihada zinafanyika kuondoa vipande hivyo.
Alisema wengine sita wanaendelea kuhudumiwa majeraha yao baada ya kufanyiwa upasuaji na hofu kubwa ilikuwa ni upungufu wa damu lakini wananchi wengi wamejitokeza kutoa damu.
“Tumepata msaada mwingine kutoka benki ya damu ya Wilaya ya Karagwe vikiwamo vifaa tiba na dawa kutoka zahanati za jirani, MSD (Bohari Kuu ya Dawa) Tawi la Muleba na ofisi ya mganga mkuu wa mkoa,” alisema Mtenjele.
Majeruhi 11 ni kati ya 42 ambao ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Kihinga waliolipukiwa na bomu la kutupwa kwa mkono, Novemba 8.
Mwanafunzi aliyekuwa amelishikilia bomu hilo lililokuwa kama chuma chakavu lilimlipukia na kufariki dunia na wenzake wengine wanne.
Pia, Shirika la Chakula Duniani (WFP) kutoka Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, jana limekabidhi Sh1 milioni kwa ajili ya majeruhi na wagonjwa wengine ili waweze kupata chakula.
Taasisi ya Tumaini Fund ya Wilaya ya Ngara nayo imechangia Sh1 milioni kwa ajili ya majeruhi hao huku Chama cha Mapinduzi (CCM) kikichangia kilo 50 za sukari.
Kutokana na michango hiyo, mkuu wa wilaya alisema vyakula hivyo vinahudumia wagonjwa wote na watavifikisha katika hospitali hiyo.
No comments:
Post a Comment