Tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa mwaka 1992, kumekuwa na maoni tofauti kuhusu utekelezaji wa sheria iliyovianzisha hasa katika awamu ya tano ambapo wanasiasa wengi wanalalamika kuminywa kwa demokrasia, kama anavyoeleza Mwenyekiti wa Chama Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashim Rungwe katika mahojiano maalumu. Endelea…
Swali: Nini maoni yako kuhusu hali ya siasa nchini
Jibu: Hali kwa sasa ni ngumu. Vyama vya siasa vimekosa uhuru wa kufanya siasa. Kulinganisha na nyuma tulikotoka. Chama kimeandikishwa kufanya siasa, unaweza kutembea pembe zote za nchi kujitafutia wabunge na wanachama, lakini sasa hivi huwezi.
Siyo vyama vipya tu, vyama vyote vimekosa uhuru wa kufanya kazi. Kama kuna kitu kimewakera mnashindwa kusema. Kwa hiyo uhuru wa vyama vya siasa umeminywa.
Swali: Lakini Rais Magufuli alisema wabunge, madiwani na wengineo wafanye mikutano kwenye maeneo yao, hilo haliwatoshi?
Jibu: Wewe lini umeshuhudia? Alisema Wabunge na wenye jurisdiction (wenye haki) mahali pale, maana kila mtu ana haki na eneo fulani. Sasa wewe huna mbunge utafanyaje siasa? Utakwenda wapi? Inakuwa vigumu.
Yeye amesema watu wenye jurisdiction, kama hauna utaulizwa, unataka kuongea nini? Wewe ni nani? Yaani hakuna uhuru.
Swali: Wewe ni mwanasheria, umeshindwa kupinga suala hilo mahakamani?
Jibu: Tume challenge lakini haiwezi kuwa hivyo.
Swali: Kwa nini msifungue kesi?
Jibu: Ndiyo tutafungua kesi, lakini kwa sasa tunazungumza.
Swali: Lakini hata kabla Rais hajazuia, hatujawahi kusikia Chaumma kikifanya mkutano wa hadhara mahali popote?
Jibu: Kwani wewe umenijuaje?
Swali: Huoni wewe ni maarufu kuliko chama chako?
Jibu: Hapana. Umenijua kwa sababu ya Chauma. Nilitembea nchi nzima wakati wa kampeni.
Chama chetu kilianza bado kikiwa kidogo wakati wa kampeni, tukatembea na wananchi wakaanza kunielewa wakati wa kampeni. Imetubidi sasa tuendelee.
Swali: Kwa nini wewe unajulikana kuliko chama chenyewe?
Jibu: Unajua mimi nina haiba yangu mwenyewe ya kufahamika na watu na chama kimebebwa na watu nyuma.
Swali: Mara ya mwisho ilikuwa lini mlipofanya mkutano mkuu na ukachaguliwa mwenyekiti?
Jibu: Mkutano mkuu ndiyo huo tuliokaa Dodoma nilipokuwa kwenye Bunge la Katiba. Kutoka tu kwenye Bunge tukaingia kwenye uchaguzi. Nilipitishwa Dodoma tulipofanya mkutano mkuu. Wakanichagua mimi nikawa mwenyekiti na viongozi wengine wapo.
Swali: Chauma kwa sasa kina wanachama wangapi?
Jibu: Tuna wanachama wengi nchi nzima.
Swali: Wangapi au hamna takwimu?
Jibu: Kwa sasa kina wanachama 5,000, maana kuandikishwa tu wanatakiwa 2,000 lazima uwapate umwonyeshe msajili.
Swali: Turudi kwenye uchaguzi, kwa nini uligombea urais huku ukijua kwamba utashindwa?
Jibu: Hapana, sikugombea nikijua nitashindwa. Kwanza kuna mambo mawili, kuki-introduce (kukitambulisha) chama kwa wananchi, unafanya kwanza advertise (tangazo), watu wakanijua, sasa ilibidi niendelee na kama nisingeendelea watu watanisahau.
Swali: Kwa mfano ingetokea umeshinda, ungeundaje Serikali?
Jibu: Hayo sasa ni mambo mengine kama yangetokea. Kwani wananchi wangenigomea kuunda Serikali? Kuna viti 10 ndani ya Bunge kwenye Katiba, ningevitumia.
Swali: Kwenye kampeni ulikuwa unatumia fedha za chama au za binafsi?
Jibu: Nilikuwa natumia fedha binafsi. Chama hakikuwa na fedha, hatupewi ruzuku sisi.
Swali: Ulitumia shilingi ngapi?
Jibu: Hiyo sasa siwezi kujua ni mpaka niangalie kwenye nyaraka.
Swali: Lakini mnatakiwa kumjulisha msajili kiasi mlichotumia, wewe ulitumia ngapi?
Jibu: Ni zaidi ya shilingi milioni 300.
Swali: Utakibeba hiki chama hadi lini, au kuna mikakati gani ya kukiinua kijitegemee?
Jibu: Hilo swali ni premature, nadhani tusubiri itakavyokuwa.
Swali: Kuna baadhi ya vyama viliungana vikaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ninyi mko upande gani?
Jibu: Mimi nilikuwa na Ukawa kule bungeni na mpaka sasa lengo letu ni moja. Hata hivyo chama chetu walitaka kwanza tukitangaze, tungejiunga na Ukawa wakati ule tusingejitangaza. Sisi hatupingani na Ukawa ni kitu kimoja, lakini katika kugombea wanachama wakasema gombea peke yako ukitangaze chama.
Swali: Tunajua kuwa urais na wabunge hamkupata. Madiwani je, mlipata?
Jibu: Hatukupata madiwani.
Swali: Kwenye Serikali za mitaa, mlipata nini?
Jibu: Kule tulipata viongozi wawili.
Swali: Kwa hiyo uchaguzi 2015 haukuwanushaisha chochote?
Jibu; Ndiyo hatukunufaika.
Swali: Kwa hiyo kama ni biashara ni sahihi kusema kwamba mlipata hasara?
Jibu: Hapana, siyo hasara kabisa, tulikuwa tunakitangaza chama na sasa kinafahamika na kinatakiwa kiendelee?
Swali: Una ushahidi gani kama chama kimefahamika?
Jibu: Ushahidi ni wewe mwenyewe unanifahamu.
Swali: Siyo kukufahamu wewe, nazungumzia chama?
Jibu: Siyo mimi, unafahamu chama. Wananchi wanakifahamu chama. Kutangaza chama hakuna limit (mpaka). Hata Chadema kilipoanza kimekaa miaka kadhaa bila mbunge. Baadaye mbunge wa kwanza akawa (Dk Walid) Kabourou. Hatuwezi kuihesabu CCM hapa kwa sababu yenyewe ilishaanza na imefahamika.
Swali: Kuna kampeni za uchaguzi wa madiwani zinaendelea sasa, ninyi mmesimamisha wagombea wangapi?
Jibu: Tumesimamisha wagombea katika mikoa ya Mtwara, Mwanza, tunao kama wanne.
Swali: Unadhani kampeni zinaendelea sawasawa?
Jibu: Kampeni zinaendelea vizuri, tutazindua mkutano wa kampeni Jumamosi mkoani Mwanza.
Swali: Tumesikia baadhi ya wanasiasa (siyo Chaumma) wanakamatwa kwa tuhuma za uchochezi katika kampeni. Hilo unalionaje?
Jibu: Mimi nafikiri ni kunyimwa uhuru wa kujieleza. Yaani mtu anataka aseme hivi anazuiliwa na polisi wanaingilia, wakitaka kumpangia cha kuzungumza. Mtu anazungumza anachojua yeye na hiyo ndiyo siasa.
Swali: Umekuwa ukisikika ukimkosoa waziwazi Rais Magufuli, lakini hujawahi kukamatwa. Unadhani ni kwa nini?
Jibu: Ni kweli ninamkosoa lakini kwa ustaarabu. Yeye ndiyo ana uamuzi, sijui, inawezekana namkosoa kistaarabu.
Swali: Kwani wewe ungechaguliwa ungewafanya nini Watanzania?
Jibu: Mimi ningewapatia chakula, mtu anatakiwa kwanza ale.
Swali: Kwani hawapati chakula?
Jibu: Hawapati, nenda kule vijijini uone mtu asikudanganye. Serikali inasema chakula kipo, lakini sisi tunaona. Maji kelele, dawa hakuna, watu wanalalamika.
Swali: Lakini si wanasema bajeti ya dawa imeongezeka na dawa zipo?
Jibu: Kuongezeka kwa bajeti hayo ni maneno ya waziri, lakini dawa hazipo.
Swali: Una maoni gani kuhusu kuongezeka kwa deni la Taifa?
Jibu: Deni la Taifa kuongezeka siyo kitu kibaya, lakini fedha zitumike kwa faida. Hata wewe ukija kwangu kama sikuamini sikupi fedha, ni mkopo. Deni lazima liongezeke, haliwezi kuwa la mwaka 1961, nchi inakua. Kuongezeka kwa deni ni kawaida, yanapanda yanashuka.
Unakuja pale wanakupa fedha, ukimaliza wanakukopesha tena, kama huaminiki sitakupa fedha. Hata mashirika kama Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani yasingetukopesha. Inatukopesha kwa sababu tuko pazuri.
Swali: Unazungumziaje vita dhidi ya ufisadi?
Jibu: Ufisadi nafikiri, Rais amezungumzia suala la ufisadi, lakini hatujaona huyo fisadi. Ni kweli amefungua mahakama ya mafisadi, lakini bado nyeupe, hatujaona mtu, mimi ni wakili sijaona. Vimekamatwa videge vidogovidogo, lakini majitu hasa waliyokuwa wanasema hatujaona.
Swali: Hao unaosema ni wadogo inawezekana wana kesi kubwa?
Jibu: Si watajwe? Hisia za nini? Tumeambiwa kule bandarini, wako wapi? Wewe unawajua? Tunataka kuwajua hawa hapa. Umekwenda kwenye bomba la mafuta hatujaona kitu.
Kwanza kuna ile lack of knowle ge (kukosa uelewa). Umekwenda umewatimua watu, lakini hawakufanya lolote wale, ni majina tu lakini hawakufanya lolote. Ni Mtanzania gani unaweza kuniambia alikwepa ushuru, nani? Mtaje hata mmoja. Unaweza? Ni hatari sana.
Swali: Vipi kuhusu mchakato wa Katiba. Leo Waziri Mkuu amesema Serikali haina fedha kuuendeleza?
Jibu: Mimi nadhani fedha siyo kitu, suala ni kwamba Watanzania wanataka Katiba mpya. Ama ianze pale ilipoishia au ianzishwe upya.
Hata kama kuna huduma za jamii, hii ni nyeti kuliko kitu chochote. Bila hivyo wananchi wanazidi kuteseka, bila Katiba mtazidi kubanwa. Katiba ndiyo msingi, tupate inayofanana na wakati tulionao, siyo Katiba ya sasa, ile tumetoka nayo kwenye mpito wa chama kimoja kuja vyama vingi. Tupate Katiba ya vyama vingi.
Zamani hata Rais alikuwa havai nguo sawasawa, sasa tumeshabadilika tunavaa sawasawa. Hakuna tena kusema Dar es Salaam kuna joto, tuko sawa. Tubadilike twende kwenye Katiba Mpya.
Swali: Kuna mbunge alitaka kupeleka muswada bungeni kuhusu mchakato wa Katiba, unadhani bunge linaweza kufanya hivyo?
Jibu: Mimi namuunga mkono huyo mbunge, lakini tutaona itakavyokuwa. Bunge kwa kiasi fulani halina uhuru wake, lakini tungoje version iletwe bungeni, tutaamua.
Maendeleo hayawezi kupatikana bila kuwa na Katiba mpya. Hii Katiba ni ya miaka ile, tulikuwa hatuzungumzi uchumi wa leo.
Swali: Katiba inahusianaje na uchumi?
Jibu: Katiba ni uhuru wa kuongea, mtu kwenda anakotaka. Lakini Katiba hii huku inatoa huku inachukua, sasa Katiba gani hiyo?
Katiba ndiyo mwongozo wa wananchi, ni sheria mama, sasa Katiba yetu haiko hivyo, tukubaliane kuwa ni ya chama kimoja.
Katiba ni ile ya Zanzibar, lakini Katiba yetu inawanyima uhuru. Tunazungumzia, oo (Waarabu) watarudi, hakuna mtu atarudi. Wewe ulishasikia mkoloni aliondoka halafu akarudi? Mara wanasema wanatumia vibaraka wao, hapana. Hayo ni mawazo yako ili ukandamize watu. Hatutaki.
Swali: Hivi karibuni Rais Magufuli amefanya mageuzi kwenye sekta ya madini na amekubaliana na kampuni ya Barrick Gold na kulipa kiasi fulani. Unaonaje?
Swali: Wale ni Barrick, sasa umepanga sheria yako mwenyewe unataka wao wafanyeje? Wao wanawekeza hapa, sasa watakaaje? Wamewekeza hela zao. Tusubiri waje wawekezaji wengine watakaokubaliana na hiyo sheria, lakini hawaji.
Swali: Nini matarajio yako ya baadaye katika siasa, utagombea tena urais?
Jibu: Mimi nafikiri mkutano mkuu utaamua, kwa sasa tuko robo ya muhula, hatuwezi kujadili leo. Tuwaachie wananchi wataamua nikiwa hai.
Swali: Lakini vipaumbele vyako kwa sasa vikoje?
Jibu: Vipaumbele nilishaleleza, wewe unakumbuka wakati ule wa Mussa, Waisrael walikwenda pale Cairo kutafuta nini? Chakula, basi.
Swali: Kwa hiyo unamaanisha nini?
Jibu: Mimi naeleza kwamba, Waisrael walifuata kwanza chakula watu washibe. Watu wana njaa hawa, hakuna Rais atakayesema kwamba mimi nataka iwe, bila wananchi kutaka. Hawa watu wanakufa. Yaani kazi na dawa.
Swali: Kwa nini unapenda kuendesha gari mwenyewe?
Jibu: Kwani mimi ni nani, mimi ni nani, nakuuliza, mimi ni nani?
Swali: Wewe ni mheshimiwa, kwa nini uendeshe mwenyewe?
Jibu: Uheshimiwa una grade zake. Kule serikalini wanatumia hela zetu wanaendeshwa. Rais anaendeshwa na mawaziri wake wanaendeshwa. Yule anayeendesha si analipwa, analipwa. Mimi nadhani hii ya kusema huyu anatembea na watu wangapi, inategemea mtu mwenyewe.