Wednesday, November 29

Walimu 12 raia wa kigeni wafikishwa mahakamani


Dar es Salaam. Walimu 12 na mkurugenzi wa Shule ya Msingi Mount Pleasant iliyopo Tabata jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matano, likiwemo la kuishi nchini kinyume cha sheria.
Waliosomewa mashtaka hayo ni Anna Ochwo; mhasibu, Josephine Nelson; Janeth Onzia; Upakmungu Nobert; Abitegeka Israel; Hajara Umavu; Sibibuka Emmanuel; Stedia Chalikunda; Evelyn Rikoba; Mkamwagi Flavia; Byamugisha Fambe; meneja, Margaret Apophia na mkurugenzi, Julius Nelson.
Mwendesha mashtaka wa Uhamiaji, Gerald Maridai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mwambapa amedai washtakiwa hao isipokuwa mkurugenzi wa shule hiyo walijihusisha na kazi bila kibali halali.
Novemba 24,2017 washtakiwa wanadaiwa wakiwa raia wa Uganda walikutwa wakifanya kazi bila kuwa na leseni au vibali vinavyowaruhusu kufanya hivyo. Pia, wanadaiwa kuingia nchini bila ya kuwa na hati za utambulisho.
Mshtakiwa Apophia anadaiwa akiwa raia wa Uganda alishindwa kufuata masharti ya hati ya kuishi nchini ambayo imemkataza kujihusisha na shughuli zozote.
Nelson, raia wa Tanzania ambaye ni mkurugenzi wa shule hiyo, anadaiwa kuajiri wahamiaji wasiofuata sheria za uhamiaji.
Baada ya kusomewa mashtaka washtakiwa waliyakana na upande wa mashtaka ulidai upelelezi haujakamilika.
Hakimu Mwambapa alimtaka kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja anayeaminika ambaye atasaini bondi ya Sh3 milioni.
Washtakiwa saba walikamilisha masharti na kuachiwa kwa dhamana, huku wengine wakipelekwa rumande. Kesi itatajwa Desemba 12,2017.

No comments:

Post a Comment