Thursday, November 23

Wadukuzi waiba habari za mamilioni ya wateja wa Uber

Uber ilifichua kwamba wadukuzi waliiba habari za mamilioni ya wateja kutoka kwa sava za kampuni hiyo ya kiteknolojia.
Kampuni ya kiteknolojia ya kuwaunganisha wasafiri na madereva wa magari, Uber, ilifichua Jumanne kwamba wahalifu wa kimitandao waliingia kwenye sava zake na kuiba nyaraka zenye ripoti kuhusu takriban wateja milioni 57.
Licha ya hudukuzi huo kutokea mwaka uliopita, maafisa wakuu wa kampuni hiyo hawakutoa habari hizo hadi sasa.
Afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo, Dara Khosrowsawi, ambaye alichukua usukani mwezi Agosti, alifichua yaliyojiri kupitia taarifa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, afisa huyo alisema habari zilizoibwa ni pamoja na majina ya wateja, anwani zao za barua pepe, nambari za simu na habari kuhusu leseni za kuendesha magari.
Aidha Khosroshawi alifichua kwamba Uber iliwalipa wahalifu hao dola elfu mia moja, hili kuharibu na kutozitumia nyaraka hizo.
Tayari kampuni huiyo imeshutumiwa vikali na wadau, ambao wanahoji kama lilikuwa jambo la busara kuwalipa wahalifu hao wa kimitandao.
Hata hivyo, afisa huyo mkuu amejiondoa kwa lawama kwa kusema kuwa hayo yalitendeka wakati wa wa uongozi wa afisa mkuu mtendaji aliyemtangulia, Travis Kalanick.
Licha ya kupanua biashara yake kwa kasi mno katika kipindi cha miaka michache, ikiwa ni pamoja na kuanzisha huduma zake katika miji kadhaa barani Afrika, kampuni ya uber imekumbwa na mizozo kadhaa katika siku za karibuni, ikiwa ni pamoja na tuhuma za udhalilishaji wa kijinsia.
Wachambuzi wa masuala ya biashara za kimataifa wamesema kuna uwezekano mkubwa kwa Uber kupelekwa mahakamani na wadau, hususan wale walioathiriwa na uhalifu huo.
Kesi nyingi tayari zimewasilishwa mahakamani zikiishutumu kampuni hiyo kuhusiana na masuala mbali mbali huku baadhi ya mamlaka za miji katika nchi mbali mbali ulimwenguni zikipinga kile zinazokiita ukiukaji wa kanuni za usafiri.
Kampuni hiyo bado inashikilia rekodi ya kapuni za kibinafsi zilizo na dhamani kubwa Zaidi duniani. Ilikadiriwa kuwa na dhamani ya dola bilioni 68.

No comments:

Post a Comment