Sunday, November 12

Wachimba makaburi wanavyoneemeshwa na watupa kafara-2


Jumapili iliyopita tuliona visa na mikasa inayowakuta watu wanaoishi au kupakana na makaburi. Tuliona jinsi baadhi ya watu wanavyotumia makaburi kufanya utapeli. Makaburi mengi ya Dar es Salaam yamejaa, lakini kuna watu wanatumia kufanya utapeli na mambo mengi yasiyofaa katika jamii. Sasa endelea.
Dar es Salaam. Rahimu Kibinja na wengine wanaofanya shughuli ya kuchimba makaburi, wakikuhadithia mambo wanayokutana nayo wakiwa kazini, unaweza kupata picha, ni kwa jinsi gani binadamu walivyofungwa vitambaa machoni na kuzibwa masikio wasizinduke dhidi ya utapeli.
Kibinja (52) anaanza simulizi yake akisema amefanya kazi ya kuchimba makaburi kwa zaidi ya miaka 30.
“Kwa sababu nina kazi katika makaburi ya Mbuyuni, twende tukazungumze katika eneo langu la kazi,” anasema Kibinja akiwa Maputo Relini katika Kata ya Azimio wilayani Temeke ambako ndiko yalipo pia makaburi ya Mbuyuni.
Anasema alianza kazi ya kuchimba makaburi huko Mtoni Tambuka Reli na wakati huo kutokana na uchache wa wakazi wa eneo hilo, shughuli hiyo ilifanyika kwa ushirikiano wa wanajamii pasipo kutoza malipo.
Kibinja anasema mwaka 1981, kutokana na ongezeko la vifo na maeneo ya makaburi kuanza kujaa, watu walianza kumtafuta kila ulipotokea msiba ili awatafutie eneo la kuzika.
“Ukitokea msiba watu wanalalamika ooh makaburi yamejaa na kujiuliza watafanyaje... baadhi wakawa wanasemezana, mwambie Kibinja. Wakiniambia eneo lilelile linalodaiwa kujaa mimi nilichimba na kuanzia hapo nikawa natafutwa popote nilipo kwa ajili ya kufanya kazi hiyo. Wakati huo nilikuwa nikiwatoza Sh3,000.”
Anasema amefanya kazi katika makaburi mengi ya Dar es Salaam na sababu kubwa ni kutokana na kufahamu taratibu za uchimbaji kwa kila imani, hivyo akiitwa na Wakristo au Waislamu hapati tabu.
“Kuzika ni jambo la heshima, hakuna anayetaka mzaha katika hilo, hivyo umakini wangu ndiyo unanitangaza na kunipa chati hapa mjini,” anasema.
Mazingira ya kazi
Kibinja anasema katika uchimbaji wa makaburi kuna wakati hukuta mabaki ya miili na changamoto hiyo ni kubwa kwa sababu watu wanazikwa kila siku.
“Sijawahi kukaa wiki sijachimba kaburi, kuna wakati nachimba hadi matano au sita kwa siku, nikikosa sana nitapata hata Kingwendu (kaburi la mtoto),” anasema.
Kuhusu hilo, Sufiani Juma (42) ambaye ni mwenzake anayefanya shughuli hizo Kinondoni Hananasif anasema amekuwa akipata kazi ya ziada ya kuzika mabaki ya miili kila anapochimba makaburi.
“Makaburi ni mengi hapa Kinondoni, si rahisi uchimbe usikute mabaki ya miili. Karibu kila mahali palishazikwa. Nimefanya kazi sasa ni miaka 13, mwanzoni nilikuwa silali hadi nilewe. Kama sijanywa usiku naota nazikwa kwenye makaburi yote niliyochimba, hivyo hata kama ni saa nane nitaamka na kwenda kutafuta pombe ilipo.”
Juma anasema alipoanza kazi alikuwa akilipwa Sh10,000 lakini sasa analipwa kati ya Sh30,000 na Sh50,000 kulingana na uwezo wa familia.
“Sijawahi kufanya kazi bure, si jambo rahisi kuchimba kaburi. Maeneo mengine ni magumu na hasa wakati wa kiangazi. Sijasoma lakini Mungu amenipa ujuzi huu,” anasema Juma.
Akisimulia maajabu ya makaburini, Kibinja anasema katika makaburi ya Mbuyuni kuna kaburi moja la ajabu ambalo likifukuliwa mwili wa marehemu unaonekana ukiwa kama ulivyowekwa.
“Amezikwa miaka 20 iliyopita, lakini kila tunapochimba ili kuandaa kaburi jingine, tunamkuta kama alivyokuwa amelala, sanda haijagusa mchanga, wala ubao aliolaziwa haujaliwa na wadudu,” anasema huku akionyesha kaburi hilo.
Ushirikina na utapeli
Kuhusu ushirikina, Kibinja anasema umekuwa ukifanyika kwa wingi makaburini na ili kuonyesha ukubwa wa tatizo anasema wapo wanaoamini kwamba hata yeye ni mganga wa kienyeji kwa kuwa tu anafanya kazi katika maeneo hayo.
Mchimba makaburi mwingine, Oswald Mwaimbo (48) anayefanya kazi Sharifu Shamba, Ilala anasema amewahi kumtibu mtu na akapona kwa imani tu ingawa yeye si mganga wa kienyeji.
“Alikuja mtu akiamini mimi ni mganga na kweli nikamlia fedha yake na nikamuita aje kunuia mwenyewe makaburini, akisema kama maiti huwa inarudi na yeye ugonjwa umrudie, kama hairudi na yeye apone, alipona kweli, lakini ni kwa imani kwa sababu sijui dawa yoyote ya kienyeji,” anasema Mwaimbo.
Kibinja anasema hata wenye kazi hiyo wanamjua, “Waganga wananiogopa, wananilinda, wananitetea kwa sababu huamini nafahamu vitu vingi kutokana na kuwaona wakifanya mambo yao, mchana na usiku.”
“Mara nyingi wananiomba niwaletee vipande vya sanda na mifupa ya watu ili wakatumie kwenye kazi zao, kama akitaka kipande cha sanda kidogo nawapa, wakitaka kikubwa nakataa, ila mifupa sijawahi kuwapa,” anasema Kibinja huku akicheka.
Kutokana na matukio ya ushirikina anasema nyumbani kwake kuku hawakauki kwa kuwa huwa anawachukua waliopelekwa makaburini kwa ajili ya kafara.
Kibinja anasema huwatumia kama kitoweo bila woga kwa sababu kuku hawana dhambi na kafara hufanyika kwenye manyoya na yeye anakula nyama.
Anasema hata akikuta wamevunja nazi huzichukua kwa sababu kafara inafanyika nje ya kifuu si ndani.
Mwaimbo anasema hajawahi kupata madhara kwa kula kuku au kuchukua nguo zinazoachwa makaburini. Anasema akipata shuka jeupe ni ‘dili’ kwani huwauzia wanaofuma na hajawahi kulalamikiwa kuwa zimeleta madhara.
“Nimewahi kufungua mbuzi, nilimkuta amefungwa na amezungushiwa dawa, nikawawahi waganga ambao nilijua muda si mrefu watakuja kuchukua mbuzi wao. Nikamfungua na nikala na familia yangu nzima, hakuna aliyeumwa hata kichwa,” anasema Mwaimbo na kuongeza kuwa amewahi kupata mwanamke kwa sababu alitaka ampatie mfupa wa binadamu akafanyie dawa.
Mwaimbo anasema mwanamke huyo alimueleza kuwa atampa chochote ili ampatie mfupa wa mtu, akamuomba wawe marafiki alikubali na akawa analala nyumbani kwake, kama mkewe hadi walipoachana.
Katika tukio jingine, Kibinja anasema, “Kuna siku nilichimba makaburi mawili jioni na tukazika usiku, ilikuwa ni wale waliofariki kwenye ajali ya wanamuziki wa bendi (jina tunalo). Tukiwa hapa Mbuyuni tunazika, kuna mwanamke aliambiwa asimame pembeni ya makaburi upande wa relini, halafu kuna mganga waliyekuja naye akasema anawaitia mzimu.”
Anasema mzimu ulioitwa hata yeye kwa mara ya kwanza na wengine waliokuwa wakishiriki shughuli ya kuzika uliwatisha kwa sababu ilikuwa mithili ya watu warefu wawili waliovaa majoho makubwa meupe.
“Baadaye ‘watoto wa mjini’ tuliokuwa pale tuligundua kuwa kuna mtu analizwa kwa sababu haikuwa mizimu, bali watu wamevishwa magongo miguuni (ngongoti).
“Walikuwa warefu na wanapoongea wananguruma, hadi leo sikufahamu walikuwa wanaongea kwenye nini, maana sauti ilikuwa na mvumo,” anasema Kibinja.
Anasema waliodaiwa kuwa mizimu walimtaka mwanamke huyo atoe kila kitu ikiwamo dhahabu alizovaa na fedha zote alizokuwa nazo.
Kibinja anasema siku iliyofuata mwanamke huyo alirudi makaburini kuutafuta mzimu akilia na kulalamika kuwa ameibiwa.
“Matukio kama hayo nimeyaona mengi, wanaofanywa hivyo mara kwa mara ni wanawake, wanaume huja mara chache na ukisikiliza kesi zao ni mambo ya kazi,” anasema.
Kibinja anasema, “Wanaokuja kujiganga kuhusu kazi ninapowasikiliza kwa makini nikiwa nimepumzika au nafanya shughuli yangu ya kuchimba makaburi wameongezeka kuanzia mwaka jana mwishoni,” anasema Kibinja.
Akisimulia anayoyashuhudia, Juma anaeleza kisa cha mwaka 2013. Anasema akiwa makaburini akifanya shughuli zake, jioni walikwenda wanaume wawili wakiwa wameongozana na vijana watatu.
Anasema wanaume hao walikuwa wakizungumza kwa lafudhi ya Kikongo na walikuwa wakiwazindika vijana hao kwa ajili ya kwenda kuchimba madini nchini Msumbiji.
“Waganga hao walijinasibu kuwa vijana hao hata wakishika majivu wakiwa mgodini yatageuka madini. Vijana walitakiwa kuweka Sh9 milioni, wakaweka hapo makaburini na wakaambiwa waondoke kinyumenyume hadi kwao,” anasimulia Juma.
Anasema siku iliyofuata ilikuwa Jumapili ambayo waganga hao walimfuata kijiweni kwake na kumuulizia iwapo anawafahamu vijana waliokuwa nao siku iliyotangulia.
“Unajua ni nini kilitokea? Waganga walikamatwa na Polisi kwa sababu fedha walizopewa na wateja wao zilikuwa bandia,” anasimulia Juma huku akicheka.
Anasema kafara zinazohusisha kuchinja mbuzi, kondoo, kuku na kuvunja nazi ni matukio ya kawaida ambayo amekuwa akiyashuhudia.
Changamoto za kazi
Kibinja anasema miaka kadhaa iliyopita aliwahi kupata homa kali akichimba kaburi akiwa chini ya ardhi futi sita.
“Kulikuwa na walimu wangu wa kazi hiyo ambao walinifundisha na walinielekeza nikipatwa na hali kama hiyo nifanye nini. Pamoja na kwenda hospitali, pia nilitumia dawa walizonielekeza wazee hao, ” anasema Kibinja bila ya kufafanua alichoelekezwa na wazee hao.
Mwaimbo anasema, “Niliwahi kupata tenda ya kuchimba kaburi, nilikuwa nimekunywa kidogo, sikumbuki vizuri alinipa hiyo tenda nani. Sikumbuki pia ilikuwaje, lakini nililala makaburini bila kujijua na nilipokuja kuzinduka nilikuwa napepesuka, marafiki, majirani na ndugu wakaniambia nimepotea kwa siku mbili.”
Anasema kila akirudisha kumbukumbu nyuma ni nani alimwambia akachimbe kaburi hamkumbuki, ingawa alizinduka kutokana na kelele za watu waliokuwa wakichimba kaburi eneo alilolala.
“Niliona kama nimelala muda mfupi uliopita, lakini nilikuwa nasikia kizunguzungu na nilikuta vifaa vyangu vya kazi vyote vipo, sikupata tiba zaidi ya “kachaso” (pombe ya kienyeji) na maisha yakaendelea,” anasema Mwaimbo.

No comments:

Post a Comment