Sunday, November 12

Rungwe: Mahakama ya mafisadi bado nyeupe


Dar es Saalam. Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashim Rungwe amesema Mahakama Maalumu iliyoundwa kwa ajili ya kusikiliza kesi za ufisadi haijafanya kazi iliyokusudiwa kwa sababu haijapata kesi za watuhumiwa wakubwa waliokuwa wakitajwa wakati wa kampeni.
Mahakama hiyo ni ahadi mojawapo ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na hata alipoingia madarakani amekuwa akiizungumzia kabla ya kujadiliwa na kupitishwa na Bunge.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Alhamisi iliyopita, Rungwe ambaye kitaaluma ni mwanasheria na wakili, alisema tangu mahakama hiyo iundwe bado ni ‘nyeupe’ haijapata watuhumiwa wa ufisadi kama ilivyokuwa ikielezwa.
“Rais amezungumzia suala la ufisadi, lakini hatujaona huyo fisadi. Ni kweli amefungua Mahakama, lakini hatujaona mtu, mimi ni wakili sijaona. Vimekamatwa videge vidogovidogo, lakini majitu hasa waliyokuwa wanasema hatujaona,” alisema Rungwe.
Akizungumza kwa hisia, Rungwe aliitaka Serikali kuwataja watuhumiwa wakubwa wa ufisadi na kuwashtaki kupitia Mahakama hiyo.
Rungwe ambaye alikuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, aliongeza, “Si wataje? Hisia za nini? Tumeambiwa kule bandarini, wako wapi? Wewe unawajua? Tunataka kuwajua hawa hapa.”
Alipoulizwa mambo mazuri ambayo anaona Rais Magufuli ameyafanya katika utawala wake wa miaka miwili, Rungwe alisema hakuna sababu ya kumsifu kwa sababu ni wajibu wake. “Mimi sijaona cha kusifu, kwa sababu yeye ana wajibu wa kutenda hayo kwa kazi aliyoomba. Ni wajibu wake. Wewe baba unaleta kuku nyumbani, kesho unaleta samaki, kuna haja ya kukusifu?” alihoji na kuongeza: “Hakuna haja ya kusifu baba anayenunua chakula kwa ajili ya watoto wake. Baba anayefanya vizuri kumpeleka mtoto shule anayotaka, sasa afanyaje? Kumsifu ni kama uzezeta fulani.”
Hata hivyo alikiri kuwapo kwa mambo mazuri yaliyofanyika japo alisema hawezi kumsifu bali kukaa kimya tu.
“Kumsifu kwangu ni kukaa kimya, pale alipoenda vizuri nanyamaza tu. Baba akikosa kuleta chakula nyumbani ni makelele. Wewe utanyamaza? Mama atanyamaza? Akileta utaona kuna amani. Akileta mikate, jelebi (andazi) na chapati, sawa tunataka kula sisi, si kusifu kwa sababu umeleta jelebi,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu kipaumbele chake kama angechaguliwa kuwa Rais, Rungwe alisema Watanzania wanahitaji kupata chakula kwanza.
“Wewe unakumbuka wakati ule wa Mussa, Waisraeli walikwenda pale Cairo kutafuta nini? Chakula, basi. Mimi ningewapatia chakula, mtu anatakiwa kwanza ale.
Akizungumzia hali ya siasa nchini, Rungwe alisema utendaji wa vyama vya siasa umekuwa mgumu kutokana na Serikali kukataza mikutano ya hadhara na maandamano kwa vyama hivyo.
“Vyama vya siasa vimekosa uhuru wa kufanya siasa. Kulinganisha na nyuma tulikotoka, chama kimeandikishwa kisheria kinafanya siasa, unaweza kutembea pembe zote za nchi kujitafutia wabunge na wanachama, lakini sasa hivi huwezi,” alisema.
Alisema tatizo hilo linaviathiri zaidi vyama visivyo na wabunge na madiwani kwa sababu havina kigezo cha kufanya mikutano kutokana na katazo hilo.
“Alisema wabunge na wengine wa kuchaguliwa kila mtu ana eneo lake kisheria. Sasa wewe huna mbunge utafanyaje siasa? Utakwenda wapi? inakuwa vigumu. Yeye amesema watu wenye jurisdiction (waliochaguliwa eneo fulani), kama hauna utaulizwa, unataka kuongea nini? Wewe ni nani? Yaani hakuna uhuru,” alisema.
Rungwe aliyeanzisha Chaumma mwaka 2012 kabla ya kugombea urais 2015 na kuambulia patupu katika nafasi za urais, ubunge na udiwani, alisema lengo la chama hicho lilikuwa ni kujitangaza.
Alisema kwa sasa wamejipanga kushiriki kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani ambako wamesimamisha wagombea wanne na watazindua kampeni hivi karibuni. Hata hivyo, taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inaonyesha Chaumma ina mgombea mmoja.
Uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 43 nchi unatarajiwa kufanyika Novemba 26.

No comments:

Post a Comment