Wednesday, November 29

Ushirikiano Afrika na Uropa

Viongozi wa Afrika watakutana na wenzao wa Ulaya katika jukwaa la ushirikiano baina ya mabara hayo mawili lakini suala tunalojiuliza kuelekea mkutano huu ni je Afrika imezidi kuwa tegemezi?

EU Afrika Gipfel in Brüssel Mohamed Ould Abdel Aziz und Herman Van Rompuy (Reuters)
Abidjan: Ushirikiano Afrika-Uropa: Je, Afrika imezidi kuwa tegemezi?
Mkutano wa tano wa ushirikiano baina ya Afrika na Ulaya  unafanyika mjini Abidjan,Cote d`Ivoire, kuanzia  tarehe 29 hadi 30 Novemba 2017. Huu ni mkutano unaowaleta pamoja viongozi, wakuu wa sera, wanamipango na wataalamu wengine kutoka mabara mawili hayo kila baada ya miaka mitatu, ili kupima mafanikio na kubaini mapungufu katika programu za ushirikiano walizojipangia.
Tangu ushirikiano huu ulipoanzishwa mwaka 2000, mikataba kadhaa imesainiwa na utekelezaji wake umekuwa ukiendelea kwa kasi ya kuridhisha na kugusa maisha ya watu wengi barani Afrka. Mambo makuu ambayo yameshughulikiwa chini ya ushirikiano huu ni kama vile usalama na amani; mifumo ya utawala bora; uhamiaji; maendeleo endelevu; upatikanaji wa nishati barani Afrika; maendeleo ya kilimo barani Afrika na uendelezaji wa ujuzi na maarifa.
Tangu mkutano mkuu wa kwanza uliofanyika mjini Cairo (2000), imekuwa ni kawaida ya mikutano hii kufanya tathmini ya yale yaliyofanyika tangu mkutano uliopita, kujua ni wapi juhudi zaidi zinahitajika na kuandaa muendelezo wa programu za ushirikiano katika miaka ijayo. Mikutano mingine mitatu imefanyika Lisbon (2007),  Tripoli (2010) na Brussels (2014).
Tansania Jenerali Ulimwengu Journalist (privat)
Jenerali Ulimwengu-Mwandishi habari
Mkutano wa mwaka huu unafanyika chini ya kaulimbinu ya ‘Vijana', ambayo ni mwafaka kabisa kwa sasa ambapo nchi zote za bara la Afrika zinabainisha ukosefu mkubwa wa ajira kwa vijana wake na vijana wanajiingiza katika mikondo ya uhamiaji haramu unaowapelekea kutumbukia katika utumwa mamboleo, kama ambavyo imeonekana miongoni mwa wahamiaji haramu wanaouzwa utumwani nchini Libya.
Kwa baadhi wa wakosoaji wa mikutano hii na ushirikiano unaojadiliwa, mkutano huu utaonekana kama kazi-bure kwani matataizo ya Afrika ni makubwa mno kiasi kwamba hayawezi kutatuliwa isipokuwa kama Waafrika wenyewe watabuni mikakati yao wenyewe itakayobadilisha jinsi nchi zao zinavyotawaliwa. Hata hivyo, waungaji mkono wa ushirikiano huuu wanabainisha kwamba mipango kadhaa ya maendeleo imeanzisha na kuendeshwa kwa ufanisi mkubwa, na kwa faida ya Waafrika.
Hapana shaka hata kidogo kwamba kiasi cha fedha zinazotengwa na Umoja wa Ulaya  ni kikubwa. Chini ya mpango unaoitwa ‘Joint Africa-EU Strategy' (JAES) ulioasisiwa mjini Lisbon mwaka 2007, hatua kubwa zimechukuliwa na mapesa mengi yamehusika.
Tunaweza kutaja machache tu, kwa mfano Pan African Programme, mpango ambao umetengewa Euro 845 milioni kwa kipindi cha 2014-2020, wakati ambapo Mpango wa Amani kwa Afrika (APF) umetengewa Euro 750 milioni. Bara la Afrika ni bara lenye umuhimu mkubwa kuliko yote katika uhusiano wa kimaendeleo na bara Ulaya. Jumla ya Euro 141 bilioni zilitengwa kwa ajili ya Afrika kwa kipindi cha 2007-13. Hii ni pamoja na kwamba Umoja wa Ulaya (EU) inagharamia kiasi cha asilimia 80 ya bajeti ya Umoja wa Afrika (AUC), mbali na misaaada inayotoa kwa jumuiya za uchumi na nchi moja moja.
Yote hii inadhihirisha umuhimu wa ushirikiano wa kiuchumi baina ya Ulaya na Afrika, lakini papo hapo inaweza kuwa kielelezo cha tatizo kubwa kwa Afrika. Labda ni jambo jema kuwa na nchi ambazo zinaweza kuzilipia nchi nyingine gharama zake, lakini ni jambo la hatari kujenga utegemezi uliokithiri.
EU Afrika Gipfel Merkel 02.04.2014 Brüssel (Reuters)
Misaada ya aina hii huwa si endelevu, kwa sababu mara nyingi hutegemea utashi na mapenzi ya asasi na mifumo ambayo Afrika haina udhibiti nayo, na misaada hiyo inaweza kukauka ghafla wakati hakuna mbinu mbadala. Uzoefu wetu wa miaka ya nyuma unaonyesha kwamba hatari hii ni ya kweli, na inashangaza kwamba leo viongozi wa Afrika bado wanarudia makosa yale yale.   
Isitoshe, bile shaka, viongozi wa Ulaya watakuwa na wakati mgumu kuendelea kutoa misaada kwa nchi ambazo haziheshimu misingi ya utawala bora, na ambazo zinazidi kubinya uhuru wa vyombo vya habari na utawala wa imla wa ‘Bwana Mkubwa' unazidi kujiimarisha.
Litakuwa si jambo la tija iwapo Umoja wa Ulaya utaendelea kutoa misaada kwa serikali ambazo zinzidi kuwanyima watu wake uhuru wa kutoa mawazo yao na tawala mabazo zinajaribu kurudisha nyuma maendeleo yaliyokwisha kupatikana katika miongo miwili iliyopita. 

No comments:

Post a Comment