Chennai, India. Ndege ya shirika la Qatar Airways iliyokuwa nusu ya safari ililazimika kutua kwa ghafla Jumapili baada ya mwanamke mmoja kubaini mume aliyekuwa akisafiri naye alikuwa akiwasiliana kimapenzi na mwanamke mwingine.
Mwanamke huyo aligundua ukosefu wa uaminifu wa mumewe baada ya kutumia kidole gumba cha mume huyo kufungua simu aina ya smartphone aliyokuwa ameishika huku akiwa usingizini.
Rubani wa ndege hiyo Na QR-972, ambayo ilikuwa inakwenda Bali, Indonesia ikitokea Doha, Qatar aliamua kuichepusha na kwenda kutua Chennai, India baada ya mwanamke huyo aliyekasirishwa na meseji za mapenzi kuzusha ugomvi, limeandika gazeti la Times of India.
Wanandoa hao na mtoto wao walikuwa wanakwenda Bali kwa mapumziko wakitokea Doha. Mwanamke huyo alianza kumpiga mumewe tena na tena na wafanyakazi wa kwenye ndege waliposhindwa kuwatuliza, rubani akalazimika kutua Chennai ambako haikuwa imepangwa kwenda.
Familia hiyo ilishikiliwa kwa muda kwenye uwanja wa ndege huo kwa vile hawakuwa na viza ya kuingia India kabla ya kupakiwa kwenye ndege nyingine kuelekea Kuala Lumpur.
“Ndege ya shirika la Qatar Airways QR-962 (Doha-Bali) imetua Chennai baada ya rubani wake kuomba akitaja sababu kuwa ni usumbufu wa abiria asiyetaka kufuata taratibu ndani,” gazeti la Hindustan Times lililoripoti kwa mara ya kwanza kisa hicho lilimnukuu ofisa wa polisi kutoka eneo hilo la viwanda (CISF).
“Mwanamke huyo na mumewe walishushwa pamoja na mtoto wao na ndege iliondoka kwenda Bali,” alisema na kuongeza kwamba ni baada ya wafanyakazi kushindwa kumtuliza mwanamke huyo aliyedaiwa kuwa raia wa Iran.
“Mwanamke huyo alifungua simu ya mumewe kwa kutumia kidolegumba cha mumewe akiwa amelala na alilipuka kwa hasira baada ya kugundua hakuwa mwaminifu,” lilisema gazeti hilo.
Familia ilibaki kwenye uwanja wa ndege wa Chennai mchana kutwa na iliondoka saa 4.30 usiku kwa ndege ya shirika la Batik Air la Malaysia.
No comments:
Post a Comment