Friday, November 10

Serikali yaikana taasisi ya mikopo elimu ya juu


Dodoma. Serikali imesema haiitambui taasisi ya Tanzania Social Support Foundation (TSSF) ambayo inajihusisha na mikopo ya elimu ya juu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema hayo leo Ijumaa Novemba 10,2017 wakati akijibu mwongozo wa Spika ulioombwa na mbunge wa Mafinga Mjini (CCM), Cosato Chumi.
 “Kuna taasisi imetoa matangazo kuwa kwa wanafunzi waliokosa mikopo watapata mikopo katika hiyo taasisi na application fee (ada ya maombi) ni Sh30,000. Napenda kufahamu u-genuine (uhalali) wa hii taasisi,” aliuliza Chumi.
Amehoji ni nini kitakachotokea iwapo wanafunzi watatoa kiingilio (ada ya maombi) hicho na mwisho wa siku ikaja kutoa mikopo kwa watu wachache zaidi.
Akijibu swali hilo, Profesa Ndalichako amesema wizara yake haiitambui taasisi hiyo na kwamba imesikitika kuona tangazo katika gazeti (hakulitaja) inayaonyesha kuwa watakuwa na shughuli ambayo mgeni rasmi atakuwa ni yeye.
“Siitambui (hiyo) taasisi, hawajanikaribisha. Nitumie nafasi hii kutoa tahadhari kwa Watanzania wawe makini kwa sababu unapoona mtu anatumia jina lako kabla hata hajafika kwako ni jambo ambalo kama Serikali nimelipokea nitalifanyia kazi ili kujua uhalali wake,” amesema.
Amesema watakaoamua kutoa Sh30,000 kujiunga na taasisi hiyo wafanye wakitambua kuwa Serikali haitambui taasisi hiyo.
Siku chache zilizopita taasisi hiyo ilitoa tangazo katika baadhi ya magazeti kuwataka wanafunzi kuomba mikopo katika taasisi yao na walipe Sh30,000 za kufanya maombi.
Taasisi hiyo ilitoa taarifa nyingine kuwataka Watanzania kuupuuza taarifa zinazosambazwa katika mitandao ya jamii kuwa wao ni matapeli.

No comments:

Post a Comment