Saturday, November 11

Trump na Putin 'waafikiana kuwashinda Islamic State nchini Syria'

Russian President Vladimir Putin (R) and US President Donald Trump (L) talk at the Apec summit on 11 NovemberHaki miliki ya pichaEPA
Image captionVladimir Putin na Donald Trump wakati wa mkutano wa Apec mnamo tarehe 11 Novemba
Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin wamekubaliana kuhakikisha kundi la wapiganaji wanaojiita Islamic State (IS) wanashindwa nchini Syria, maafisa wa rais wa Urusi wamesema.
Ikulu ya Urusi imesema taarifa imeandaliwa na wataalamu baada ya viongozi hao wawili kukutana kwa muda mfupi pambizoni mwa mkutano wa viongozi wa nchi za Asia na Pasific nchini Vietnam Jumamosi.
Kwa jumla, viongozi hao wawili walikutana mara tatu katika kipindi cha saa 24 katika mji wa Da Nang.
Hakujakuwa na thibitisho lolote rasmi kutoka kwa Marekani kuhusu tamko hilo la Urusi.
Mkutano kati ya Rais Trump na Vladimir Putin ulitarajiwa kufanyika wakati wa mkutano huo wa Apec, lakini ni maelezo machache sana ambayo yametolewa.
Wawili hao walikutana kwa mara ya kwanza Julai katika mkutano wa G20 katika mji wa Hamburg nchini Ujerumani.
Donald Trump na Vladimir Putin wakiwa Danang, Vietnam, 10 Novemba 2017Haki miliki ya pichaREUTERS
Image captionWawili hao walisimama pamoja wakiwa wamevalia shati zilizofanana wakati wa picha ya pamoja Ijumaa
Maswali kuhusu uhusiano wa Donald Trump na Urusi yamekuwa yakiulizwa mara kwa mara.
Wasaidizi wake wakuu wa zamani wanachunguzwa kwa tuhuma za kushirikiana na Urusi kuingilia uchaguzi wa urais wa Marekani wa mwaka 2016.
Urusi imekanusha tuhuma hizo.
Ingawa White House haijasema chochote kuhusu mkutano wa wawili hao, taarifa ya Kremlin iliyotolewa Jumamosi imesema viongozi hao "waliafikiana kwamba mzozo wa Syria hauwezi kutatuliwa kwa njia ya kijeshi".
Kadhalika, walikariri "kujitolea kwao kuwashinda Isis [jina jingine la IS]" na kuzitaka pande zote kushiriki mazungumzo ya amani ya Geneva.
Vladimir Putin na Donald Trump wakiwa Apec 11 NovembaHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionWawili hao walionekana wakizungumza wakati wa kupigwa picha ya pamoja
Kwa mujibu wa shirika la habari la Interfax la Urusi, wameahidi kuendelea kudumisha njia za mawasiliano za kijeshi kati ya majeshi ya Urusi na Marekani kuzuia uwezekano wa kushambuliana wakati wakishambulia IS>
Urusi imekuwa ikiunga mkono serikali ya Bashar al-Assad katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka sita sasa.
Marekani nayo huwasaidia waasi wa makundi ya Waarabu wa Syria na Wakurdi.
Tangu 2014, Marekani imeongoza muungano ambao umekuwa ukitekeleza mashambulio ya kutoka angani dhidi ya IS nchini Syria.

No comments:

Post a Comment