Benki ya NMB imetoa Sh 500,00 na kumfungulia akaunti mwanafunzi huyo wa shule ya Sir John ikiwa ni kumpongeza kwa kuwa wa kwanza katika matokeo ya mtihani wa kitaifa wa darasa la saba nchini mwaka huu
Akizungumza leo Novemba 11 ,Meneja wa NMB Tawi la Madaraka, Victor Msofe amesema kuwa akaunti aliyofunguliwa mwanafunzi huyo ni aina ya Chipukizi ambayo itamsaidia katika kununua mahitaji yake muhimu awapo shule ya Sekondari.
“NMB Tawi la Madaraka tumefurahishwa sana kusikia taarifa kuwa mwanafunzi wa kwanza kitaifa ametoka Jijini Tanga, ni faraja kwa mkoa na wateja wetu kwa ujumla hivyo tukaona tumuunge mkono kwa kumfungulia akaunti” amesema Msofe.
Meneja huyo amesema hatua hiyo ya NMB ina lengo la kuwahamasisha wanafunzi wengine iwe wa shule za msingi au Sekondari kufanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa na kuwataka wadau wengine kumchangia kwa kutumia akaunti hiyo .
Hadija ameishukuru NMB kwa kumfungulia akaunti na kubainisha kuwa imempa nguvu na ari ya kufanya vizuri zaidi kwenye masomo ya Sekondari.
“Akili na mawazo yangu yote hivi sasa yapo kwenye masomo, nafikiria nitakwenda kusoma shule gani, na huko lengo langu ni kuhakikisha naongoza mitihani yote ili nifikie lengo langu la kuwa daktari baadaye” amesema Hadija.
Mama wa mwanafunzi huyo, Jane Kihiyo ameshukuru NMB kwa kumpa nguvu mtoto wake huyo na kusisitiza kwamba tukio la kumfungulia akaunti limewafurahisha.
Mtaalamu wa masuala ya bima jijini Tanga, Ramadhani Manyeko amewashauri wadau wa elimu kuangalia uwezekano wa kumtafutia shule itakayoweza kuendeleza kipaji chake cha akili darasani bila kujali ni ya Serikali au binafsi.
“Kwa nchi za wenzetu Hadija na wenzake walioshika nafasi ya pili hadi tano wangekuwa ni lulu kubwa, wangetafutiwa shule zenye uwezo wa kuwaendeleza vipaji vyao bila kujali ni ya Serikali au binafsi kwani ni faida kubwa kwa Taifa na wangelipiwa gharama zote ili wasome bila usumbufu” amesema Manyeko.
No comments:
Post a Comment