Rais Donald Trump wa Marekani ameiweka Korea Kaskazini kwenye orodha ya Mataifa yanayofadhili ugaidi, na kutishia kuimarisha zaidi vikwazo dhidi yake, lakini waziri wa mambo ya nje amesema bado diplomasia inayo nafasi.
Kwa tangazo hilo la Rais Trump, Korea ya Kaskazini imeongezwa kwenye orodha ya nchi ambazo Marekani inazichukulia kama wadhamini wa ugaidi duniani, ambayo tayari inazo Iran na Syria. Rais huyo amewashambulia tena watangulizi wake, akisema anayoyafanya leo yalipaswa kufanywa miaka mingi iliyopita.
Mbali na kuishutumu Korea Kaskazini kuendesha mpango haramu wa nyuklia na makombora, vile vile Donald Trump amesema nchi hiyo inaendesha mauaji nje ya ardhi yake, ingawa hakuna visa vya mauaji kama hayo vinavyojulikana kufanywa na serikali ya mjini Pyongyang, mbali na kile kilichomuuwa kaka wa kiongozi wa sasa Kim Jong-un.
Akitangaza uamuzi wake katika kikao cha baraza la mawaziri mjini Washington, Trump amesema baada ya mchakato mzima kukamilika, Korea Kaskazini itakabiliwa na vikwazo vikali kabisa. Amesema, ''Hatua hii inaongeza vikwazo na adhabu kwa Korea Kaskazini na watu wenye mafungamano na nchi hiyo, na itasaidia kuitenga kabisa nchi hiyo inayoongozwa na serikali ya wauaji, kama ambavyo mmekuwa mkisoma na wakati mwingine mkiandika.''
Trump ameongeza kwamba kuwa kuanzia Jumatano wizara ya mambo ya nje itatangaza vikwazo vya ziada, vikali kabisa dhidi ya Korea Kaskazini, na kwamba mchakato huo utadumu kwa wiki mbili.
Tillerson atofautiana na Trump
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari baada ya tangazo la Rais Trump, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson amesema Marekani bado ina matumaini kwamba mchanganyiko wa vikwazo na juhudi za kidiplomasia unaweza kutumiwa kumshawishi kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un kuja kwenye meza ya mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia wenye utata.
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong un, ambaye waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson amesema vikwazo vimemziba mdomo
Tillerson amesema tayari wanazo taarifa kwamba vikwazo vya bidhaa za petroli ambavyo China imeikea Korea Kaskazini vimeanza kuporomosha mapato ya Korea Kaskazini. ''Ni kutokana na athari hizo kwamba nchi hiyo haijafanya tena uchokozi wake kwa muda wa siku 60 zilizopita,'' amesema Tillerson, akimaanisha Korea Kaskazini.
Hata hivyo, wachambuzi wanasema hatua hii ya Trump dhidi ya Korea Kaskazini ni ya kiishara tu, kwa tayari Marekani imeiwekea nchi hiyo vikwazo chungu nzima.
Korea ya Kaskazini imeizoea orodha hiyo
Hii sio mara ya kwanza Marekani kuiweka Korea Kaskazini katika kundi linalofadhili ugaidi. Nchi hiyo inayoongozwa kwa usiri mkubwa ilikuwa tayari kwenye orodha hiyo hadi mwaka 2008, wakati Rais George W Bush alipoiondoa kwenye orodha hiyo, ili kuweka shinikizo zaidi kwa nchi nyingine ambazo zilikuwa haziibani vya kutosha Korea Kaskazini.
Wataalamu wanaamini kuwa Korea Kaskazini kwamba katika muda wa miezi kadhaa, Korea Kaskazini itapata makombora ya masafa marefu yanayoweza kufyatuliwa kutoka bara moja na kutua bara jingine, yakiwa na uwezo kufanya mashambulizi dhidi ya Marekani. Ikulu ya Rais Donald Trump imesema kamwe haitairuhusu Korea Kaskazini kupata uwezo huo.
No comments:
Post a Comment