Mahakama ya Juu ya Kenya, Jumatatu imetoa uamuzi kuwa Rais Uhuru Kenyatta alichaguliwa kihalali katika zoezi la marudio ya uchaguzi wa urais uliyofanyika Oktoba 26.
Kenyatta alipata zaidi ya asilimia 98 ya kura katika uchaguzi uliosusiwa na Muungano wa Upinzani.
Majaji wote sita waliosikiliza kesi hiyo wameamua kwa kauli moja kwamba Kenyatta alichaguliwa kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini humo, IEBC, waliojitokeza kupiga kura walikuwa chini ya asilimia 39 ya Wakenya milioni 19.6 waliojiandikisha.
Mgombea wa upinzani, Raila Odinga, ambaye alijitoa kwenye kinyang'anyiro hicho, aliwataka wafuasi wake kususia uchaguzi huo, na waandamanaji waliwazuia maafisa wa tume ya uchaguzi kufungua vituo vya kupigia kura katika ngome za upinzani. Odinga alisema uchaguzi huo ulikuwa ni aibu.
Maombi ya walalamikaji watatu yaliwasilishwa kwenye mahakama hiyo, na yote yametupiliwa mbali.
No comments:
Post a Comment