Ndugai ameunda kamati hizo baada ya zingine mbili za kutathmini mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya Tanzanite na almasi kuwasilisha taarifa kwa Rais John Magufuli Septemba,2017 na kusababisha baadhi ya mawaziri kujiuzulu.
Akitangaza kamati za sekta ya uvuvi na gesi bungeni mjini Dodoma leo Ijumaa Novemba 17,2017, Spika Ndugai amemrejesha Dotto Biteko aliyeongoza kamati iliyochunguza Tanzanite kuwa mwenyekiti wa kamati itakayochunguza sekta ya gesi.
Mussa Zungu alikuwa mwenyekiti wa kamati iliyochunguza almasi na sasa ni mjumbe katika kamati ya uvuvi.
Ndugai akitangaza kamati hizo amesema anatumia kanuni ya 5(1) ya Kanuni za Bunge toleo la 2016 ambayo inampa madaraka ya kuziunda kwa kadri atakavyoona inafaa.
Amesema kumekuwa na hali ya kusuasua kwa sekta hizo, ukiwemo uvuvi wa bahari kuu. Amesema sekta hiyo inachangia pato la Taifa kwa asilimia 1.4 ambayo ni sawa na Sh3.2 bilioni wakati kuna zaidi ya Sh400 bilioni ambazo zinapotea bure.
Spika Ndugai amewataja wajumbe wa kamati ya sekta ya uvuvi itakayoongozwa na Anastazia Wambura kuwa ni Zungu, Salum Mwinyi Rehani, Masoud Salim Abdalla, Tauhida Nyimbo, Mbaraka Dau, Dk Immaculate Semesi, Dk Christina Ishengoma, Stanslaus Mabula, Mussa Mbarouk na Cosato Chumi.
Kamati ya sekta ya gesi itaundwa na Innocent Bashungwa, Dastan Kitandula, Dk Seleman Yusufu, Wanu Hafidhi Ameir, Oscar Mukasa, Ruth Mollel, Richard Mbogo, Omari Kigua, Abdallah Mtolea na Sebastian Kapufi.
Spika Ndugai amemwagiza Katibu wa Bunge kuwawezesha wabunge hao ili waanze kazi na kamati zimetakiwa kufanya kazi ndani ya siku 30 tangu siku watakayokabidhiwa majukumu yao.
No comments:
Post a Comment