Muhina ambaye ni mwongozaji watalii katika hoteli hiyo, alikuwa aondoke na ndege ya Coastal Aviation saa nne asubuhi lakini viongozi wa hoteli walimbadilishia ndege, hivyo aliondoka na Air Exel iliyofika salama Serengeti.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Novemba 17,2017 Meneja Uendeshaji wa hoteli ya andBeyond Serengeti UnderCanvas, Mussa Matala amesema Muhina ambaye anasomeka kwenye orodha ya ndege kama Maina alikuwa apande ndege hiyo lakini waliamua kumbadilishia ili awahi kazini.
Amesema waliomba aondolewe kwenye orodha ya wasafiri wa ndege hiyo lakini kwa bahati mbaya hadi ndege ilipoondoka jina lake lilikuwepo.
Wakati huohuo, raia watano wa kigeni ambao walifariki dunia katika ajali ya ndege ya Coastal Aviation, akiwemo rubani, Dewald Raubenheimer raia wa Afrika Kusini, ambaye kwenye orodha ya awali ya waliofariki jina lake halikuwepo inatarajiwa kusafirishwa Jumapili Novemba 19,2017.
Mhudumu wa chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, Francis Costa amesema miili mitatu kati ya 11 imechukuliwa na ndugu.
Amesema miili iliyochukuliwa ni ya ndugu wawili waliokuwa wakurugenzi wa Masai Wondering, Nasibu na Shatri Mfinanga. Mwingine ni wa Joyce Mkama ambaye alikuwa mfanyakazi wa hoteli ya Serena.
"Uchunguzi wa miili ya wageni kutoka nje ya nchi unaendelea na ukikamilika itasafirishwa kwa mazishi katika nchi za Afrika Kusini, Ujerumani na Italia," amesema.
Ndege hiyo namba 5H-EGG aina ya Cessna Grand Caravan ilianguka baada ya kugonga kingo za creta ya Empakai, umbali wa mita 3,250 kutoka usawa wa bahari ikitoka Kilimanjaro kwenda Hifadhi ya Serengeti.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo amesema uchunguzi unaendelea kuhusu ajali hiyo.
No comments:
Post a Comment