Thursday, November 9

Sekta binafsi, za Umma watakiwa kushirikiana


Dar es salaam. Rais mstaafu Benjamin Mkapa  amesisitiza kuwa bado kuna umuhimu wa sekta ya umma na binafsi  kufanya kazi  kwa pamoja ili kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini.
Mkapa ambaye pia ni Mwanzilishi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Benjamin  Mkapa Foundation  (BMF) inayowajengea uwezo watumishi wa afya na kuboresha huduma za afya.
Rais huyo mstaafu ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Novemba 9 katika mkutano wa nne wa wadau wa taasisi hiyo ulioandaliwa kwa kushirikiana na Benki M.
Amesema bado kuna mapungufu kwenye baadhi ya maeneo hususani katika sekta ya afya na zingine, hivyo ameshauri ziwepo jitihada  za makusudi kati ya sekta zote mbili kushirikiana katika kutekeleza mikakati ya maendeleo endelevu.
"Kupitia makubaliano haya sekta ya umma na binafsi yatasaidia kutengeneza mazingira  sahihi ya kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuboresha Mpango Mkakati wa Maendeleo wa Mwaka 2025,"amesema Mkapa.
Pia amewataka wadau wa maendeleo nchini kuendelea kushirikiana na serikali katika kutekeleza mikakati ya maendeleo hususani mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini.
Awali akifungua mkutano huo, Naibu Waziri  wa Nchi, Ofisi  ya  Rais (Tamisemi), Josephat Kandege amesema  BMF ina zaidi ya muongo mmoja sasa na imekuwa taasisi  yenye nguvu na inayounga mkono juhudi za Serikali za kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya hasa maeneo ya vijijini.
 "Wote tumeshuhudia kazi kubwa na nzuri inayofanywa na BMF na inaendana na vipaumbele vya kitaifa, sera pamoja na mikakati  mingi inayolenga kuboresha huduma za kupambana na ukimwi, uzazi na rasilimali watu wakiwamo wahudumu wa afya "amesema  Kandege.
"Tunahitaji kuangalia tija ya watumishi waliopo kwa kuboresha maslahi na mazingira  bora ya ufanyaji kazi. Hivyo tunahitaji  kuangalia namna gani tutaongeza tija kwa wafanyakazi kwa kupitia ubunifu wa nia mbalimbali.
"Hivyo basi naiasa BMF pamoja na taasisi nyingine zinazofanya shughuli  kama hii kulifanyia kazi suala hili ili kuja na  mbinu za kuongeza tija kwa watumishi hasa wa sekta ya afya,"amesema  Kandege.
Mbali na hilo, Kandege  ametumia nafasi  hiyo kuziagiza halmashauri zote nchini kushirikiana kwa karibu na wadau wa maendeleo ambao wana nia ya kusaidia na  Serikali kuboresha huduma za afya.
Pia  Kandege amezitaka taasisi mbalimbali  za maendeleo kujitokeza kwa wingi kusaidiana na Serikali katika kuboresha sekta ya afya.
Hata hivyo, Kandege  amesema Serikali bado inakiri bado haijafanya vizuri katika eneo la afya ya uzazi na kwamba takriban wajawazito 8,000 hupoteza maisha .
"Hili halikubaliki kwa kuwa vifo vingine vinazuilika na katika kutatua changamoto  hii, Serikali  na wadau tushirikiane kutekeleza mpango mkakati wa afya ya uzazi, mama na mtoto,"amesema Kandege.

No comments:

Post a Comment