Wednesday, November 15

Ridhiwani, Msigwa wavutana bungeni


Dodoma. Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwan Kikwete na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa, leo Jumatano, wamerushiana maneno bungeni kila mmoja akionyesha ubabe wa kutunga sheria.
Hayo yalijitokeza wakati Bunge lilipoketi kama kamati chini ya mwenyekiti wa Bunge, Najma Murtaza Giga kupitia vifungu vya muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa 2017.
Muswada huo ambao ulichangiwa na wabunge wawili tu,mmoja wa CCM na mwingine kutoka kambi ya upinzani uliwasilishwa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju.
Hali hiyo ilijitokeza baada ya Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Ruth Mollel kushikilia msimamo wa kuwepo usawa wa kijinsia katika muundo wa bodi ya mfuko wa fidiwa kwa wafanyakazi.
AG Masaju alipendekeza bodi hiyo na iwe na wajumbe tisa wakiwamo wawakilishi wawili wawili wanaowakilisha vyama vya waajiri vyenye wanachama wengi kwenye mfuko huo wa fidia.
Pia alipendekeza wajumbe wawili wawili wanaowakilisha vyama vya wafanyakazi vyenye wanachama wengi kwenye mfuko na wakili wa Serikali kuanzia ngazi ya mwandamizi atakayemwakilisha AG.
Wajumbe wengine ni mwakilishi wa wizara yenye dhamana ya Hifadhi ya Jamii, Mwakilishi wizara ya Fedha, mwakilishi wizara ya Tumishi wa Umma na mwakili wa Jumuiya ya watu wenye ulemavu.
Hata hivyo, Mollel aliwasilisha jedwali la marekebisho, akipendekeza muundo huo uzingatie jinsi ya kike badala ya kuliacha suala hilo katika utashi wa mtu mmoja ambaye atakuwa anateua.
Pamoja na AG Masaju kueleza madhara ya kuingiza kifungu cha aina hiyo katika sheria, bado mbunge huyo alisimama katika msimamo wake na kutoa hoja kuwa Bunge lijadili suala hilo.
Ndipo mwenyekiti alipomruhusu Ridhiwan kuchangia na aliposimama alisema yeye amesimama sio kuunga mkono hoja ya Mbunge huyo bali kutoa maoni yake kuhusiana na uandishi wa sheria.
“Sina hakika sana kama mama yangu (Ruth) ni mwanasheria. Katika uandishi wa sheria nchi hii hakuna sheria inayoandikwa kwa kuzingatia gender (jinsi). Hilo la kwanza tuelewane,”alisema.
“Unapoweka kipengele chochote kile kwamba iwe kipengele hiki kimzungumzie mtu huyu awe mwanamme ni tayari kuna mtu (mwanamke) umeshambagua,”alisisitiza na kuongeza;-.
“Unaposema kipengele hiki kiwe mwanammke maana yake kuna watu tayari umeshawatenga. Kinachotakiwa ni busara ya wale wanaoteua sio jambo la kuandika gender,”
Hata hivyo, Mchungaji Msigwa alipopewa fursa alisema itakuwa ni makosa makubwa kutoingiza kipengele hicho na kurudi nyuma kwenye historia ya jinsi mwanamke alivyofanywa kama “object”.
“Ni wakati sasa hivi wa wanawake kuamka ili kuhakikisha mnatetea haki zenu ili tufikie kiwango kile cha  50-50 hata tunapotunga sheria. Mfano mzuri ni ile sheria inayomlazimisha Rais kuteua wabunge”.
Mchungaji Msigwa alisema sheria hiyo inamlazimisha Rais kuteua angalu nusu ya wabunge wawe wanawake na kuna wakati Rais John Magufuli alighafulika na kuteua wabunge wengi wanaume.
Hali ndani ya ukumbi wa Bunge ilikuwa kama ifuatavyo:
Ridhiwan: Mwenyekiti Taarifa
Msigwa:Hatutoagi taarifa kwenye kuchangia
Ridhiwani: Leo ndio unapewa taarifa hapa leo. Wanataka kutuyumibisha bwana. Hatuwezi kuyumbishwa bwana sisi tunatengeneza sheria.
Msigwa: Hata mimi natengeneza sheria
Ridhiwani: Hakuna namna hiyo Msigwa bwana. Hatuwezi kutunga sheria ambazo ziko biased (zina pendelea)
Mwenyekiti wa Bunge: Waheshimiwa wabunge. Naomba mkae nyinyi nyote wawili Naomba mkae  wote wawili. Mheshimiwa AG Tuendelee.
Ridhiwan: Sie tumesoma sheria bwana
Mwenyekiti wa Bunge: Mheshimiwa Stella Manyanya (Naibu Waziri wa Elimu)
Stella Manyanya: Kwanza nataka kumuambia Bwana Msigwa . Si vyema kutumia vibaya kumtaja mheshimiwa Rais kwa mambo ambayo sio lazima sana. Kwa mfano kumwambia alimuondoa mbunge”
Naibu Waziri huyo alimtaka Mchungaji Msigwa asipitilize katika suala hilo akisema kama Mbunge alijiuzulu mwenyewe ni vyema akasema hivyo, kuliko kusema Rais ndiye aliyemuondoa.
AG Masaju alipopewa kuchangia mjadala huyo alianza kwa kusema,“namshukuru sana mheshimiwa Ridhiwan Kikwete ametusaidia kuweka suala hili vizuri. Ukirudi kwenye uandishi wa sheria”
“Tunayo sheria ya kwanza kabisa inayoitwa sheria ya tafsiri ya sheria. Yenyewe ndio msingi wa tafsiri ya sheria zote  na ndio muongozo wa kutafsiri sheria,”.
“Mbona kwenye sheria inasema HE (mwanamme) lakini wanawake wamo humo ndani. Tunao muongozo mahsusi unaotuongoza katika kuandika sheria,”alisisitiza Masaju.
Mollel alipopewa fursa ya kuhitimisha hoja yake, alisema amesikitishwa sana na jinsi hoja hiyo ilivyochukuliwa akisema yeye akiwepo serikalini waliweka utaratibu wa usawa kwa wote.
Mwenyekiti aliamua suala hilo liamuliwe kwa kura, ambapo baada ya kuwahoji wanaoafiki hoja ya Mbunge huyo waseme Ndioo na wasioafiki waseme Sioo, waliosenda Sioo wakashinda.
Muswada huo ulipitishwa na Bunge kuwa Sheria na sasa unasubiri sahihi ya Rais Magufuli ianze kutumika.

No comments:

Post a Comment