Wednesday, November 29

Praljak: Mhalifu wa kivita afariki baada ya kunywa sumu mahakamani The Hague

Slobodan Praljak in court at The Hague, 29 NovemberHaki miliki ya pichaICTY
Kikao cha kusikiliza rufaa iliyowasilishwa na washtakiwa wa uhalifu wa kivita mjini The Hague, Uholanzi kimesitishwa ghafla baada ya mmoja wa washtakiwa kusema amekunywa sumu baada ya kusikiliza hukumu.
Slobodan Praljak, 72, alikuwa mmoja wa viongozi sita wa zamani wa kisiasa na wa kijeshi wa Bosnia wa asili ya Croatia ambao walikuwa wamefika mahakamani.
Amefariki akitibiwa hospitalini na Umoja wa Mataifa umesema sasa mahakama hiyo ni "eneo la uhalifu".
Alikuwa amehukumiwa kufungwa jela miaka 20 mnamo 2013 kwa makosa ya uhalifu wa kivita yaliyotekelezwa katika mji wa Mostar.
Baada ya kusikiliza hukumu kwamba majaji walikuwa wamedumisha kifungo hicho, alimwambia jaji, "Nimekunywa sumu".
Sita hao walikuwa wanasikiliza uamuzi wa mwisho wa rufaa uliokuwa unatolewa na mahakama maalum ya kimataifa ya UN iliyokuwa inashughulikiwa makosa yaliyotekelezwa Yugoslavia (ICTY).
Ingawa walikuwa washirika dhidi ya Waserbia wa Bosnia wakati wa vita hivyo vya 1992-95, Wacroatia wa Bosnia na Waislamu walipigana wenyewe kwa wenyewe kwa miezi 11.
Mji wa Mostar ulishuhudia mapigano makali zaidi.
'Usiondoe gilasi'
Praljak alisimama na akainua mkono wake hadi kwenye kinywa chake, kisha anainamisha kichwa chake nyuma na kuonekana kunywa kitu kutoka kwenye gilasi ndogo.
Jaji mwandamizi Carmel Agius mara moja alisitisha shughuli na gari la kuwabeba wagonjwa likaitwa.
"Sawa," jaji alisema. "Tunaahirisha ki...Tunaahirisha...Tafadhari, pazia. Usiondoe gilasi ambayo ameitumia alipokunywa kitu."
Kabla ya pazia kurejeshwa, ukumbi wa mahakama umeonekana kujawa na mkanganyiko, anasema mwandishi wa BBC Anna Holligan kutoka The Hague.
Gari la kuwabeba wagonjwa lilionekana baadaye likifika nje ya ukumbi wa mahakama huku helikopta ikipaa juu angani.
Wafanyakazi kadha wa uokoaji wameingia ukumbini na vifaa vyao.

Uhalifu dhidi ya Waislamu

Praljak, kamanda wa zamani wa wahudumu wakuu wa Jeshi la Walinzi wa Wacroatia wa Bosnia (HVO), alifungwa kwa makosa ya jinai dhidi ya binadamu.
Baada ya kufahamishwa kwamba wanajeshi walikuwa wanawakamata Waislamu Prozor majira ya joto 1993, alikosa kuchukua hatua zozote za maana kuzuia hilo, mahakama hiyo ya UN ilisema.
People take pictures in front of Mostar's Old BridgeHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionDaraja la kale la Mostar baada ya kukarabatiwa
Aidha alikosa kuchukua hatua hata baada ya kupashwa habari kwamba mauaji yalikuwa yamepangwa, pamoja na mashambulio dhidi ya wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa na kuharibiwa wka daraja la kale la mji wa Mostar na misikiti.
Mahakama ya ICTY ambayo iliundwa 1993 itamaliza kati yake mwisho wa mwaka huu.

No comments:

Post a Comment