Monday, November 27

Picha za wagonjwa kulala chini zamshangaza waziri


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema uchakavu wa Zahanati ya Kata ya Bujonde iliyopo Wilaya ya Kyela umetokana na uzembe wa halmashauri.
Ummy ameyasema hayo leo Jumatatu baada ya picha mbalimbali kusambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha mandhari isiyo rafiki kwa wagonjwa wanaotibiwa katika zahanati hiyo.
Mwananchi imezungumza na waziri ambaye amelitolea suala hilo ufafanuzi na kushangazwa kwa nini vitanda 25 vilivyotolewa halmashauri havijafikishwa katika zahanati hiyo.
"Nimepokea! Nitawasiliana na mwenzangu wa Tamisemi mhe Suleiman Jafo ili achukue hatua mara moja! Lakini hapa mimi naona ni uzembe wa halmashauri husika! Wameshindwa kufanya ukarabati wa zahanati hii au kujenga mpya? Amehoji.
Ummy amehoji ni kwa nini wameshindwa kununua vitanda, kwani mwaka huu wamepeleka bure ikiwa ni kukamilisha ahadi ya Rais ya kununua vitanda vya wagonjwa 25 katika kila halmashauri nchini.
Hata hivyo, Ummy amesema halmashauri inatumiwa pesa za dawa, vifaa na vifaa tiba kutoka serikalini kupitia MSD/Wizara ya Afya na Mfuko wa Pamoja wa Afya.

“Hizi fedha wao wanapeleka wapi? Vipi kuhusu mapato ikiwemo kutoka kwa wananchi wanaochangia kupata huduma za matibabu? Kipaumbele chao ni nini kwenye matumizi ya mapato yao ya ndani? Amesema Ummy akiahidi kuchukua hatua za haraka kunusuru wakazi wa eneo hilo.

No comments:

Post a Comment