Saturday, November 4

Nasa waibua mjadala wakitaka eneo la Pwani kujitenga



Mombasa, Kenya. Baadhi ya wanasiasa na viongozi wa Muungano wa National Super Alliance (Nasa) eneo la Pwani wameibua mjadala wakitaka eneo hilo kuondolewa katika ramani ya Kenya.
Wanasiasa takriban 18 wameituhumu Serikali katika awamu zilizopita na ya sasa ya Jubilee inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake, William Ruto wakidai zimekuwa zikipuuza matakwa yao.
Kenya iliongozwa na Jomo Kenyatta ambaye ni baba yake Rais Uhuru, baadaye Daniel  Arap Moi aliyetawala kwa kipindi cha miaka 24.
Utawala wa awamu ya tatu ulikuwa chini ya Rais Mwai Kibaki kuanzia mwaka 2003 hadi 2012 alipoingia Rais Uhuru.
Wanasiasa hao wa Pwani wakiongozwa na Gavana wa Mombasa, Ali Hassan Joho na mwenzake wa Kilifi, Amason Kingi wamesema wameanza mazungumzo kuhakikisha eneo hilo linaondolewa kutoka katika ramani ya Kenya.
Pia, wanapinga uchaguzi wa marudio wa urais uliofanyika Oktoba 26,2017 uliompa ushindi Rais Uhuru.
"Safari ya kuiondoa Pwani kutoka Kenya imeanza, tutatumia njia zote kisheria za hapa nchini na kimataifa kuhakikisha tumefikia lengo hilo," amesema Gavana Joho alipozungumza na waandishi wa habari mjini Mombasa.
Mbali na mawakili, amesema wanashauriana na wakazi wa Pwani wakiwamo; viongozi wa kidini, wa vijiji na vijana ili suala hilo lisionekane ni la wanasiasa na viongozi pekee.
"Tunaelewa safari hiyo haitakuwa rahisi, lakini sharti tufikie shabaha yetu," amesema.
Alichosema Kingi
Kauli ya Joho ilienda sambamba na ya Gavana Kingi wa Kilifi ambaye amesisitiza kuwa hawafi moyo kwa suala hilo.
"Umefika wakati wa kuinusuru Pwani. Tumepuuzwa kwa muda mrefu sana," amesema.
Awali, suala la wanasiasa wa Pwani kutaka kuondoa maeneo hayo kutoka kwenye  ramani ya Kenya lilipuuzwa na kiongozi wa Nasa, Raila Odinga.
Waziri mkuu huyo wa zamani alisema haungi mkono pendekezo hilo na kwamba halitawezekana.
Kwa sasa kinachosubiriwa ni iwapo Raila atazungumza lolote kuhusu suala hilo.

No comments:

Post a Comment