Wednesday, November 15

Muswada wa Fao la kujitoa kusomwa bungeni


Dodoma. Hatima ya Fao la Kujitoa ambalo limekuwa kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi, sasa iko mikononi mwa Bunge wakati Serikali itakapowasilisha Muswada ya kuiunganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),George Masaju ameliambia Bunge leo Novemba 15 kwamba  Muswada wa kuiunganisha Mifuko hiyo, utasomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Bunge unaomalizika kesho kutwa.
Kwa mujibu wa AG Masaju, suala la Fao la Kujitoa litafikiriwa katika Muswada huo wa Sheria, na kama suala hilo halitakuwamo kwenye Muswada huo, basi wabunge ndio watakaoamua.
Masaju ametoa  kauli hiyo wakati akijibu hoja ya Mbunge wa Temeke (CUF), Abdalah Mtolea, aliyehoji kwanini Serikali imewasilisha marekebisho mepesi ya sheria, wakati Fao la Kujitoa ni kilio kikubwa.
Mtolea aliibua suala hilo wakati akichangia Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali  namba 4 wa mwaka 2017, uliowasilishwa Bungeni na AG Masaju na kupitishwa na bunge hiyo jana.
Mbunge huyo amesema walitarajia Serikali ingeleta Muswada wa kuiunganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kama ambavyo Rais John Pombe Magufuli, ameonyesha kukerwa na utitiri wa mifuko hiyo.
“Vitu vingi ambavyo tumetegemea Serikali ingevileta hapa hawajavileta wameleta vitu vyepesi vyepesi. Mheshimiwa Rais kila siku anapiga kelele kwamba ana kerwa na utitiri wa hii mifuko,” alisema.
“Amelisema hili (Rais) mara kadhaa na AG ndio watu wa kumsaidia Rais katika kuhakikisha wanaharakisha mchakato wa kupunguza hii mifuko ya hifadhi uwe mmoja au miwili,”
Amesema tangu Rais atoe kauli hiyo, ana taarifa kuwa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), imefanya tafiti na kufanya maandalizi ya kuwasilishwa kwa Muswada huo.
“Tulitarajia muswada huo unaletwa leo hapa mambo hayo hayapo. Kila siku waheshimiwa wabunge hapa wanapiga kelele kuhusu fao la kujitoa,” amesema Mbunge huyo na kuongeza
“Wananchi wanapiga kelele wanalalamika kwanini wananyimwa fursa ya kujitoa kwenye mifuko ya Jamii hadi watimize miaka 55.  Wachukue fedha zao waende wakafanye shughuli nyingine”.
“Mtu ameshafanya kazi miaka yake 10 anaona kwamba kilichopo kwenye mifuko ya Jamii kinamtosha kufanya mtaji. Kinamtosha kutengeneza kiwanda chake unamzuia”
“Miaka 55 ni muda wa uzee ni muda wa kula mafao na muda wa kupumzika. Tunataka fedha sasa hivi ili tuweze kuwekeza ili wakifika miaka hiyo 55 wawe wameshakuwa matajiri”
Hata hivyo akijibu hoja hiyo, AG Masaju alisema alichowasilisha ni marekebisho ya sheria ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi na sio Muswada wa Marekebisho ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
“Kwenye masuala makubwa ya kisera yanayoletwa na muswada mahsusi sio unaoletwa na AG kwa ajili ya marekebisho ya sheria ambazo zimeleta shida katika utekelezaji wake”.
“Nishauri hata hii hoja ya kwamba ingetegemewa ingekuja hapa muswada mahususi kwa ajili ya kuunganisha mifuko ya Hifadhi ya  Jamii, hii nayo isingeweza kuletwa kwenye muswada huu”
“Imekuwepo mifuko mingi wewe mwenyewe umesema kwamba ni ya utitiri, unaileta yote pamoja unaunganishwa upi na upi  na utakuja na skimu gani,” amesema na kuongeza;
“Naomba kushauri Bunge lako tukufu kuwa katika mkutano huu wa Bunge  wa Bunge linaloendelea sasa, muswada huu wa  mfuko wa Hifadhi utasomwa kwa mara ya kwanza kwenye bunge hili”
“Pamoja na mambo mengineyo utahusika pia na hiyo hoja ambayo ameisema ya Fao la kujitoa itakuwa considered (litafikiriwa ) wakati huo. Kama haitakuwamo mtaamua nyinyi wenyewe wabunge”.
 “Serikali inafanya kazi kwa makini sana na naomba kuwashukuru wabunge nyinyi kuweni imara, kuweni macho muisaidie Serikali na kuishauri lakini mutoe ushirikiano mzuri kwa Serikali.
“Hii ya sheria inayounganisha mifuko ya Hifadhi ya Jamii itasomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano huu wa bunge lako linaloendelea,” amesisitiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Suala la Fao la Kujitoa, limekuwa likiibuka karibu kila mkutano wa Bunge, huku baadhi ya vyama vya wafanyakazi navyo vikitishia kuchukua hatua za kisheria endapo Fao hilo la Kujitoa halitarejeshwa.
Juzi suala hilo liliibuka tena Bungeni, lakini Naibu Spika, Dk Tulia Ackson akasema kwa anavyofahamu kwa sasa na kwa msimamo wa sheria, Fao la Kujitoa lilishafutwa na sheria.

No comments:

Post a Comment