Monday, November 13

Museveni: Kufanya masihara ni kosa kubwa


Hoima, Uganda. Rais Yoweri Museveni amesema kuwa watu wanaomchukulia kimasihara wanatenda “kosa kubwa” akitolea mfano namna alivyotendewa na chama tawala wa cha Uganda People’s Congress (UPC) miaka ya 1980.
Rais Museveni alitoa mfano wa mambo yaliyo nyuma ya pazia alivyopambana na watu wa nje kuhusu nini cha kufanya kibiashara na hazina kubwa ya mafuta itakapogundulika wazi.
Alisema muda mfupi baada ya kushika madaraka mwaka 1986, baadhi ya wazurungu kutoka Ulaya walimfuata ili awaidhinishe kufanya kazi ya utafutaji na uchimbaji mafuta nchini Uganda.
Museveni alisema, hata hivyo, aliwakatalia na badala yake aliamua kuwapeleka Waganda kusomea uchumi wa mafuta na gesi ili kujenga uwezo wa ndani kabla ya kuanza kazi ya uchimbaji.
“Mimi sitaniwi,” alisema Rais. “Hata UPC walifanya kosa hilo.”
Mwaka 1980, Museveni ambaye aligombea urais kwa tiketi ya Uganda Patriotic Movement (UPM) alionya kwamba atakwenda msituni ikiwa uchaguzi utavurugwa. Milton Obote alishinda hivyo akarudi kuiongoza Uganda kwa mara ya pili baada ya kupinduliwa na Idi Amin mwaka 1971.
Museveni alianzisha vita vya msituni dhidi ya serikali ya Obote iliyopinduliwa na Tito Okello Lutwa ambayo pia ilipinduliwa na Museveni Januari 1986.
Rais akizungumza Jumamosi iliyopita wakati wa sherehe fupi za uzinduzi wa ujenzi wa bomba la mafuta katika Mradi wa Bomba la Mafuta Afrika Mashariki, alitaja umuhimu wa kubuni vyanzo vya uchumi na akasema wanaofanya masihara naye wanatenda kosa kubwa.

No comments:

Post a Comment