Monday, November 13

Mmiliki wa shamba lililofutwa asema JPM amedanganywa



Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela 
Tanga. Shamba la mkonge la Mnazi wilayani Lushoto lililotangazwa leo Jumatatu na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela kuwa limefutwa na Rais John Magufuli  kutokana na kutoendelezwa limezua utata baada ya aliyekuwa  akilimiki kudai kwamba hajawahi kulitelekeza.
Mkurugenzi wa kampuni ya Le-Marsh Enterprises Ltd iliyokuwa
ikiendesha shamba hilo, Lawarence Macharia amedai kuwa Rais Magufuli amedanganywa kwa sababu hadi mwaka jana kati ya hekta 1,460 zilizopo hekta 900 alishakuwa amepanda mkonge.
Ametoa takwimu hizo alipokuwa akizungumza na Mwananchi mara baada ya Shigela kutangaza rasmi kwamba Rais amefuta umiliki wa kampuni ya Le-Mash Enterprises katika shamba la mkonge la Mnazi wilayani Lushoto.
Shigela ambaye alikuwa akifungua mkutano wa “Mkonge Day” uliohudhuriwa na wadau kutoka mikoa mbalimbali nchini amesema kuwa Rais amelirejesha serikalini shamba la Mnazi na kuelekeza kuwa maombi yafanyike upya na kwamba lisibadilishwe matumizi bali watakaochukua wahakikishe
wanazalisha zao la mkonge.
“Kwa taarifa hii nakaribisha rasmi maombi kwa watakaokuwa na uwezo wa kuzalisha mkonge katika shamba la Mnazi, nitatoa maelekezo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ya namna ya kuendesha mchakato kwa watakaokuwa na uwezo wa kulichukua shamba hilo,” amesema Shigela katika
mkutano huo.
Baada ya tangazo hilo, Mwananchi ilizungumza na Macharia ambaye alikuwepo kwenye mkutano huo na kueleza kushangazwa kwake kusikia taarifa hizo na kubainisha kuwa Rais amedanganywa kuhusiana na shamba la Mnazi huku akisisitiza amenyang’anywa kwa sababu za kisiasa.
“Wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015, mbunge aliwaambia wapigakura akishida atahakikisha kuwa shamba hilo linanyang’anywa na watagawiwa mashamba ya kulima mahindi na mazao mengine,” amesema
Macharia.

Amesema  Oktoba 27 mwaka jana aliandikiwa barua na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mnazi akiambiwa kuwa kampuni yake imeshafutiwa usajili wa shamba hilo na kwamba asikanyage shambani hapo.

Amesema hadi sasa ameshapanda hekta 537 za mkonge mpya, hekta 147 zikiwa na mkonge wa zamani na hekta 216 zililimwa upya kwa ajili ya kupanda mkonge mwingine na kwamba kampuni yake ilitarajia kuuza nje ya nchi tani 425 za singa.
“Hata hivyo, nimefurahishwa na taarifa kwamba Rais ameelekeza lisibadilishwe matumizi kwa sababu mkonge una faida kubwa katika uchumi wa viwanda,” amesema Macharia na kusisitiza kuwa atafuataili ili aweze kurejeshewa shamba hilo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Mkonge(SAT), Deogratius Ruhinda amesema wadau wameonyesha kuridhishwa baada ya kusikia kuwa Rais ameamuru shamba la Mnazi lisibadilishwe matumizi ya kilimo cha Mkonge.

No comments:

Post a Comment