Rais wa Uganda Yoweri Museveni, amewaambia wanachama wa muungano wa madaktari nchini humo kwamba ataitisha hali ya dharura na kuwakamata madaktari wote iwapo wataendelea na mpango wao wa kufanya mgomo wa kitaifa wiki ijayo.
Kiongozi wa muungano huo ameambia BBC kwamba matamshi hayo yalitolewa katika mkutano siku ya Jumanne .
Lakini katibu wa maswala ya habari katika afisi ya rais Museveni amekana kutoa matamshi kama hayo.
Kulingana na mwandishi wa BBC Catherine Byaruhanga rais Museveni aliingilia kati ili kuzuia kile kinachoonekana huenda ikawa tatizo la kitaifa iwapo madaktari wote katika hospitali za uma na vituo vya afya watafanya mgomo.
Daktari Ekwaro Obuku, kiongozi wa muungano huo amesema kuwa rais Museveni alimuonya na wenzake kwamba ataitisha hali ya dharura na kuwakamata madaktari wote iwapo watafanya mgomo huo siku ya Jumatatu.
Lakini katibu wa maswala ya habari katika afisi ya rais Museveni amekana kutolewa kwa vitisho hivyo na kusisitiza kuwa mkutano huo ulikuwa mzuri.
Daktari Obuku anasema kuwa wasiwasi wa rais ulionyesha umuhimu wa madaktari hao.
Kulingana na daktari huyo rais Museveni aliwaahidi kutathmini upya mishahara ya madaktari na kufanya mikutano zaidi kuhusu swala hilo.
Muungano huo sasa utapiga kura nyengine siku ya Jumatatu kuona iwapo wataendelea na mgomo huo.
Madaktari wanalalamikia mishahara duni pamoja na uhaba wa dawa na vifaa ambavyo wanasema vinasababisha vifo ambavyo vinaweza kuzuiwa.
Mfanyikazi wa umma anayelipwa mshahara wa juu nchini Uganda analipwa zaidi ya dola elfu moja za Marekani kwa mwezi.
No comments:
Post a Comment