Sunday, November 12

Mradi wa maji Moshi kugharimu Sh400 milioni


Mradi wa majisafi na salama katika vijiji vya Mweka, Sungu na Chuo cha Wanyamapori Mweka unaotarajiwa kukamilika Februari mwakani utagharimu Sh400 milioni na kunufaisha zaidi ya kaya 3,500.
Akizungumza katika mahojiano na mwandishi wa gazeti hili, Kaimu mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Moshi (Muwsa), John Ndetiko alisema: “Kiutendaji eneo hili la Kibosho siyo letu, ila kwa kuwa wizara ya maji imetuomba tushirikiane na Halmashauri ya Moshi, Bonde la Pangani na Sekretarieti ya Mkoa, tukaona ni vyema tuutekeleze ili tuwasaidie wananchi hawa ambao wanaoumia zaidi ni wanawake.”
Mhandisi wa maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Elifadhili Mrutu alisema wakati wanaanza walikutana na changamoto ya hitaji kubwa la wananchi wa eneo hilo.
Mrutu alimuomba mkuu wa mkoa huo kuwaeleza wananchi hao kuwa mradi huo ni mali yao na wanapaswa kuupokea na kuutunza.
“Wakati wa upimaji wananchi walipinga sisi kuendelea, lakini tulivyomshirikisha mkuu wa wilaya, alifika na kuitatua changamoto hiyo...nazidi kuwaomba wananchi waupokee na kuutunza kwa manufaa ya vizazi vijavyo,” alisema Mrutu.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Sungu, William Kiwale alisema baada ya wataalamu kutoka Bonde la Maji la Pangani kufika na kupima kiwango cha maji waligundua kuwa yaliyopo yanatosheleza kaya 3,600 kijijini hapo.
“Wataalamu walipofika kwenye chanzo cha Mto Lombanga waligundua kuwapo kwa kiasi cha kutosha cha maji, wakapendekeza kutoa lita 10 kwa sekunde. Tunaomba Serikali iendelee na mradi huu,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira aliwataka wananchi kushirikiana na wataalamu wanaoendelea na mradi huo.

No comments:

Post a Comment