Dar es Salaam. Rais John Magufuli leo anatimiza miaka miwili tangu alipoapishwa kuongoza Taifa la Tanzania, lakini kipindi hicho kinaweza kuelezewa kuwa ni cha mchakamchaka kwa Serikali ya Awamu ya Tano, wanasiasa wa chama tawala na upinzani, wafanyakazi, wafanyabiashara na watu wengine.
Kama mwananchi hakukimbizwa mchakamchaka na utimuaji wa wafanyakazi hewa, basi alikumbana na sakata la vyeti vya kughushi; na kama si kamatakamata basi alisikia nidhamu sehemu za kazi ikiwa imerejea.
Kwa upande mwingine kama waziri alipona kutumbuliwa, alikumbana na mchakamchaka wa kutakiwa atekeleze majukumu yake kwa wakati.
Hali hiyo pia ilikuwa kwa wafanyabiashara ambao wale waliopona katika msako wa wahusika wa biashara ya dawa za kulevya, walikumbana na msako wa wakwepa kodi.
Serikali pia ilijikuta katika mchakamchaka wa aina yake. Pale ilipofanikiwa kudhibiti biashara ya madini, ilikumbana na utaifishaji wa ndege, pale Jeshi la Polisi lilipokamata wanasiasa wa upinzani, ilijikuta ikifanya kazi ya ziada kuuaminisha umma kuwa inachukua hatua dhidi ya watekaji, washambuliaji na kikundi cha “watu wasiojulikana”.
Yote hayo yanafanya kipindi cha miaka miwili ya Rais John Magufuli kuweza kuelezewa kwa kifupi kama “miaka miwili ya mchaka mchaka”.
Miaka hiyo miwili ya kwanza katika awamu ya kwanza ya uongozi wa Rais Magufuli, imekuwa na mambo chanya na changamoto zake; ya kufurahisha na ya kuchukiza; ya furaha na huzuni; ya chuki na upendo na ya kukatisha tamaa na ya matumaini.
Lakini katika kipindi hicho, Rais Magufuli amefanya mengi ya kuandaa mazingira ya kuelekea katika uchumi wa viwanda kama alivyosema katika hotuba inayochukuliwa kuwa ni dira ya uongozi wake aliyoitoa bungeni Novemba 20, 2015, takriban siku 15 baada ya kuapishwa.
Baada ya mwaka uliopita kushughulika na masuala kama wafanyakazi hewa, ununuzi wa ndege, vyeti vya kughushi, utumbuaji wa watumishi wa umma, utengenezaji wa madawati, na utekelezaji wa elimu bure, mwaka huu Serikali ilijikita katika masuala mengine makubwa, hasa usafirishaji wa mchanga nje, ikichunguza mikataba, sheria na biashara ya madini.
Rais aliagiza makontena 270 yaliyokuwa yakisubiri kusafirishwa nje kwa ajili ya kuyeyushwa ili kupata mabaki ya madini kama dhahabu na shaba, yazuiwe na kuunda kamati mbili ambazo zilichunguza na kubaini udanganyifu uliokuwa unafanywa na kampuni ya Acacia, inayomiliki migodi ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara.
Kamati ya kwanza ilibaini kuwa kiwango cha dhahabu iliyomo kwenye mchanga unaosafirishwa nje ni mara kumi ya kile kilichotangazwa na Acacia na kubaini ukiukwaji wa sheria katika uendeshaji wake, wakati kamati ya pili ilibaini kuwa kampuni hiyo haikuwa imesajiliwa na kwamba ilikuwa inakwepa kodi.
Sakata hilo, pamoja na madini ya Tanzanite na almasi, lilisababisha baadhi ya mawaziri kuachia ngazi na hivyo Rais kufanya mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri.
Pia limesababisha watendaji wakuu wawili wa Acacia kuachia ngazi, huku kampuni ya Barrick Gold, inayomiliki asilimia 64 ya hisa za Acacia, ikikubali kulipa fidia ya Sh700 bilioni kuonyesha “nia njema”, hali kadhalika kukubali Serikali imiliki asilimia 16 ya hisa huku faida ikiwa ni asilimia 50 kila upande baada ya waendeshaji migodi kutoa gharama za uendeshaji.
Pia umesababisha Rais kuamua kujenga ukuta wa kuzunguka migodi ya madini ya Tanzanite ili kudhibiti wizi.
Mwaka huu pia ulishuhudia Serikali ikizindua awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa reli ya kati inayojengwa kwa kiwango cha standard gauge, ambayo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria na mizigo mingi zaidi, huku ikiwa na kazi kubwa. Awamu hiyo itahusu usafiri kati ya Dar es Salaam na Morogoro.
“Reli hii itarahisisha usafiri wa abiria na mizigo ndani ya nchi na kwenda nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, itazalisha ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 600,000 na itasadia kuimarisha uchumi,” alisema Rais Magufuli wakati akizindua ujenzi huo.
Pia, Rais Magufuli na Yoweri Museveni wa Uganda walizindua ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Tanga hadi Hoima nchini Uganda, ikiwa ni urefu wa kilomita 1,443 huku zaidi ya kilomita 1,100 zikiwa Tanzania.
Wakati hayo yakiendelea, Serikali imeendelea kudhibiti matumizi yake kwa kudhibiti safari za nje, ikiongozwa na Rais Magufuli ambaye hadi sasa ametembelea nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki tu pamoja na Ethiopia.
Kwa upande wa afya, changamoto bado ni kubwa lakini Serikali ilipiga hatua kubwa baada ya kuongeza kwa takriban mara mbili, bajeti ya dawa katika mwaka huu wa fedha.
Hata hivyo, Serikali imeendelea kukosolewa kutokana na kuendelea kupiga marufuku mikutano ya hadhara, maandamano na kuongezeka kwa kasi ya kufungia magazeti, hali inayolalamikiwa kuwa ni kuendelea kuminya uhuru wa habari.
Katika uamuzi wake wa mwisho, Serikali ililifungia kwa miezi mitatu gazeti la Tanzania Daima kwa madai kuwa habari yake kuhusu idadi ya watu walioambukizwa ugonjwa wa Ukimwi ilikuwa inapotosha.
Lakini taarifa ya kufungiwa kwake imejaa hoja za habari kadhaa zilizowahi kuandikwa na gazeti hilo, ikizielezea kuwa ni za uchochezi.
Masuala mengine ambayo ni mwendelezo wa mikakati iliyoanza mwaka jana ni pamoja na mikopo ya wanafunzi, ambayo Serikali imetoa fedha mapema ili kuondoa usumbufu uliotokea mwaka jana na utekelezaji wa kuhamishia makao makuu mkoani Dodoma.
Lakini masuala mengine yaliyoikimbiza nchi mchakamchaka ni pamoja na mauaji ya viongozi wa vijiji katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji ambako zaidi ya watu 30 waliuawa katika matukio tofauti.
Tofauti na mauaji ya kawaida ya vijijini ambako hufanyika kwa kutumia silaha za jadi, katika wilaya hizo za Mkoa wa Pwani wauaji walitumia silaha za moto na Jeshi la Polisi halijawahi kutamka kuwa limekamata watuhumiwa wakiwa hai zaidi ya kusema limedhibiti na kuua baadhi katika mapigano.
Mwaka huu pia ulitawaliwa na malalamiko dhidi ya vitendo vya utekaji, baada ya baadhi ya wanasiasa kulalamikia kuchukuliwa na maofisa wa usalama huku wasanii wakitekwa.
Lakini tukio baya zaidi lililosababisha huzuni kwa jamii ni shambulizi dhidi ya mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye alirushiwa takriban risasi 30 wakati akiwa kwenye gari nje ya makazi yake mjini Dodoma.
Lissu, ambaye hivi sasa anatibiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya, alishambuliwa mchana wakati akiwa ametoka bungeni kuhudhuria kikao cha asubuhi.
Hadi sasa, Jeshi la Polisi halijaeleza kama limemkamata mtu yeyote likimuhusisha na shambulio hilo.
Lissu ni mmoja wa wanasiasa waliokumbana na kamatakamata ya polisi mwaka huu kabla ya shambulio hilo na ameshtakiwa mahakamani kwa kesi kadhaa.
Viongozi wengine waliokumbana na kamatakamata hiyo ni pamoja na wabunge wa vyama vya upinzani, madiwani na wenyeviti wa wilaya na mikoa, tukio la hivi karibuni likimuhusisha kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliyekamatwa mapema wiki hii.
Tukio jingine ni la kushambuliwa kwa ofisi ya mawakili ya IMMMA Advocates, ambayo inaendesha kesi kadhaa za kibiashara na kisiasa, zikiwemo zinazomkabili Lissu.
Matukio hayo na mengine yalianzisha kilio cha chinichini cha kudai Katiba mpya, ikikitoka ndani na nje ya CCM na kusababisha aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu kujiuzulu ubunge.
Nyalandu, ambaye ameomba kujiunga na Chadema kuunganisha nguvu za kudai demokrasia, amekuwa mtu wa kwanza katika utawala wa Rais Magufuli kukihama chama tawala, akiwa mbunge.
No comments:
Post a Comment