Wednesday, November 29

Maswali kibao magari yasiyo na mwenyewe bandarini

Rais John Magufuli akiwa Bandari ya Dar es
Rais John Magufuli akiwa Bandari ya Dar es Salaam alipofanya ziara ya kushtukiza juzi na kukuta magari 53 ya kubebea wagonjwa na 50 ya Jeshi la Polisi yaliyokwama bandarini hapo kwa muda mrefu. Picha na Emmanuel Herman 
Dar es Salaam. Hatua ya Rais John Magufuli kushtukia uwepo wa magari 103 yaliyokwama katika Bandari ya Dar es Salaam kwa tariban miaka miwili baada ya kufanya ziara ya kushtukiza juzi imeibua maswali mengi.
Baadhi ya maswali hayo ni nani aliagiza magari hayo, kwanini hafahamiki, kwanini yamekaa muda mrefu bandari, kwanini yameandikwa kuwa ni ya ofisi ya rais?
Katika bandari hiyo, Rais aliyaona magari madogo ya kubebea wagonjwa 50 yaliyokwama tangu Juni 29, 2015 na magari ya Jeshi la Polisi 53 yaliyopo tangu Juni 2016.
Mbali na magari hayo, Rais Magufuli pia alibaini uwapo wa magari yaliyotekelezwa bandari hapo kwa zaidi ya miaka 10 hali inayopunguza uwezo wa bandari kuhifadhi mizigo. Kufuatia hali hiyo, alitoa siku saba kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Jeshi la Polisi kumpa taarifa juu ya sababu za magari hayo kukwama kwa muda mrefu na kinyume cha sheria.
Pia, Rais aliagiza magari yote ambayo yamekaa bandarini hapo kwa muda mrefu yaondolewe kwa taratibu za kisheria na kwa uwazi.
Hiyo siyo mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza katika bandari hiyo. Machi 23 mwaka huu, alifanya ziara ya kushtukiza na kushuhudia makontena 20 ya mchanga wa madini alioagiza usisafirishwa nje ya nchi tangu Machi 2.
Katika ziara hiyo, pia alikutakontena moja likiwa na magari matatu ambalo nyaraka zilionyesha kuwa lilikuwa na nguo za mitumba.
Julai 2, wakati Rais Magufuli akihutubia katika uzinduzi wa upanuzi wa badari hiyo, alisema anazo taarifa ya kuwapo kwa vichwa 15 vya treni vilivyoshushwa hapa lakini havina mwenyewe.
Hatua hiyo ya Rais Magufuli kushtukia uwapo wa magari hayo juzi imezua maswali kadhaa yakielekezwa katika idara za Serikali ikiwamo TRA, TPA na mawaziri husika katika idara hizo. Miongoni mwa maswali yaliyoibuka ni nani aliyeagiza magari hayo? Je, ni mtu binafsi au ni taasisi za Serikali?
Kwa kwa kuwa magari hayo yaliagizwa mwaka 2015 wakati ambao Rais alikuwa Jakaya Kikwete na mengine mwaka 2016 baada ya Rais huyo kuondoka, ni sehemu ya magari 777 yaliyoagizwa kabla ya kiongozi huyo kuondoka?
Oktoba 20, 2015 Rais Kikwete alilikabidhi Jeshi la Polisi magari 399 mapya kati ya 777 yaliyoagizwa ili kufanikisha shughuli ya uchaguzi.
Swali lingine ni kwa nini yawe na anuani ya ofisi ya Rais? Kwa muundo wa ofisi ya Rais ni ‘taasisi’ kubwa inayohusisha idara mbalimbali zikiwamo wizara kama Tamisemi pamoja na Utumishi na Utawala Bora inayobeba idara kama Takukuru na Usalama wa Taifa (TISS).
Je, ni taasisi gani iliyohusika kuagiza magari hayo miongoni mwa hizo? Je, inawezekana waagizaji wa magari hayo waliandika ofisi ya Rais ili kuviogopesha vyombo vya dola kuyafuatilia?
Swali jingine linaloibuka ni kuhusu muda tangu magari hayo yalipotua bandarini ikiwa ni muda mfupi tangu Rais Magufuli kuingia madarakani hadi alipoyagundua siku chache zilizopita.
Swali jingine ni kuhusu mawaziri na watendaji wa Serikali waliokuwapo katika ziara ya Rais Magufuli kushindwa kujibu maswali. Je, mawaziri hao hawajui lolote kuhusu magari hayo? TPA na TRA hawakujua lolote kuhusu magari hayo kwa kipindi hicho?
Akizungumza na Mwananchi kwa simu kuhusu uingizwaji wa magari bandarini, naibu rais wa Chama cha Wakala wa Forodha Tanzania (Taffa), Edward Urio alisema haiwezekani mzigo uletwe bandarini halafu mwenyewe asijulikane.
“Haiwezekani mzigo ufike bandarini halafu usiwe na mwenyewe kwa sababu kila mzigo unaposhushwa bandarini unakuwa na manifest inayoonyesha muagizaji, msafirishaji na mpokeaji,” alisema Urio.
Hata hivyo, alisema kuna mizigo ambayo inakuwa ya biashara na hivyo kutolewa kwake hutegemea kupatikana kwa wateja, hivyo muagizaji anatakiwa kuingia mkataba na benki hadi mzigo utakapouzwa.
“Wakati mwingine mzigo unaweza kufikishwa bandarini mteja akawa anatafutwa, huo mzigo utawekewa ‘to order’ na muagizaji ataingia mkataba na benki ili kumdhamini hadi mzigo uuzwe.
“Kwa mfano mtu ameleta mbolea na hajapata wateja, anadhaminiwa na benki hadi mzigo uuzwe kisha watagawana na hiyo benki.”
Aprili mwaka huu, Rais Magufuli akizindua mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam alisema kuna vichwa vya treni 11 vilishushwa katika bandari hiyo, lakini mmiliki wake hajulikani.   

No comments:

Post a Comment