Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mfuko wa udhamini wa kudhibiti Ukimwi umetoa Sh660 milioni kwa Wizara ya Afya ambazo zitanunulia dawa hizo na Sh2 milioni zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha Mererani kilichopo mkoani Manyara.
Amesema kituo hicho mbali ya huduma za afya, kitatumika kutoa huduma za dawa za kufubaza VVU kwa watu waishio na virusi vya Ukimwi na pia, kitatumika kuelimisha jamii ili kujiepusha na maambukizo mapya.
"Kwa mara ya kwanza mfuko wa udhamini wa kudhibiti Ukimwi ulianza kazi Oktoba 21,2017, hivyo Serikali itaendelea kutenga fedha za mfuko na kuhakikisha inahamasisha wananchi, wadau ikiwemo sekta binafsi kuchangia," amesema Majaliwa wakati wa ufunguzi wa kongamano la kitaifa la maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani leo Novemba 28,2017.
Pia, ametaka bodi ya mfuko huo na watendaji wake kuhakikisha wanasimamia kikamilifu fedha ziweze kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amesema kuna changamoto ya ushiriki wa wanaume kupima virusi vya Ukimwi kuwa mdogo kulinganisha na wanawake.
Amesema wanaume wamekuwa wakutaka wanawake wakapime na matokeo yake wanapoanza kuugua wanakuwa wamechelewa kupata matibabu.
Pia, amesema wengine ambao hupima huwa wagumu kwenda kuchukua dawa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Dk Leonard Maboko amesema mikoa yenye kiwango kikubwa cha maambukizo ya VVU ni Njombe, Iringa na Mbeya pia kwenye machimbo kama vile Mererani.
No comments:
Post a Comment