Thursday, November 9

Magufuli awatoa hofu watanzania deni la Taifa


Wakati deni la Taifa likitajwa kuongezeka, Rais John Magufuli amesema hali hiyo isiwashangaze watanzania kwa sababu kuwa na madeni inaonyesha imani ya mataifa makubwa kwa nchi ya Tanzania juu ya uwezo wa kulipa.
Pia, amesema kiwango cha mikopo ni kidogo ukilinganisha na mataifa mengine ya Afrika.
Akizungumza jana na wananchi wa Misenyi mkoani Kagera alipotembelea kiwanda cha Sukari cha Kagera, Rais Magufuli alisema kiwango kilichofikiwa ni cha kawaida.
Juzi akiwasilisha mapendekezo ya mpango wa maendeleo ya Taifa na mwongozo wa mpango na bajeti kwa mwaka huu wa fedha 2018/19,Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema deni limeongezeka kwa asilimia 17.
Dk Mpango alisema miradi mitano ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa na serikali imechangia ongezeko la asilimia 17 la deni la Taifa ambalo ni zaidi ya Dola 26.115 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh57.453 trilioni).
“Ongezeko hilo linachangiwa na mikopo mipya iliyochukuliwa ili kugharamia miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), Strategic Cities, Mradi wa Usafirishaji Dar es Salaam (Dart) na kupanua upatikanaji wa maji safi Dar es Salaam,” alisema.
Rais Magufuli ambaye ametimiza miaka miwili tangu aingie madarakani, alisema kuongezeka kwa deni hilo kunatokana na baadhi ya mikopo iliyodumu kwa muda tangu awamu zilizopita.
“Watu wanasema Serikali inakopakopa sana. Tajiri yoyote lazima akope na ukishakopa maana yake unaheshimika, mtu ambaye hawezi kukopesheka ina maana haaminiki,’
Alisema pamoja na deni hilo Tanzania imekopa asilimia 32.5 ya GDP na imeruhusiwa kukopa hadi asilimia 56 ya GDP.
“Kukopa na kuwa na madeni si dhambi, madeni mengine tunahangaika nayo leo hii yalikopwa tangu enzi za Mwalimu Nyerere,” alisema
Alisema suala la msingi ni kuangalia ni namna gani fedha hizo zinavyotumika na kwamba fedha zote zimeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa barabara pamoja na reli.
Pia aliwataka wawekezaji wa viwanda vya sukari kuweka mikakati ya kuziba pengo la upungufu wa tani 130,000 kwa mwaka ili azuie bidhaa hiyo kuagizwa kutoka nje.
Akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha sukari cha Kagera Rais Magufuli alisema lengo lake ni kuzuia sukari kutoka nje baada ya kuhakikishiwa ongezeko la uzalishaji viwandani.
Alisema kuwa mahitaji kwa mwaka ni tani 440,000 na kuwa serikali iko tayari kuvisaidia viwanda ili viongeze uzalishaji ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa mikopo kutoka benki ya kilimo nchini. Ametaka kiwanda cha Kagera kuongeza uzalishaji hadi tani 75 kwa mwaka tofauti na sasa ambapo wanazalisha kati ya tani 65 na 67 kwa mwaka na kuagiza wapewe mkopo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji.
Pia aliagiza viwanda vinavyoagiza sukari kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya bidhaa kufanyiwa uhakiki kwa kuwa huagiza zaidi ya mahitaji na kiasi kingine kuingizwa sokoni kwa ajili ya matumizi ya majumbani kuwa ni ukiukaji wa taratibu unaohatarisha afya.
Aidha ameagiza kuondolewa kwa watumishi ndani ya siku tatu wanaohusika na utoaji wa vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi kuwa wapangiwe kazi nyingine kwa kuwa kuna mianya ya rushwa.
Pia alisema Tanzania itaendelea kujikopesha kwenye taasisi mbalimbali za fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kuwa inakopesheka na kufanya hivyo sio kosa.

No comments:

Post a Comment