Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Dk Revocatus Ndyekobora amesema kati ya majeruhi hao, wanafunzi ni 42 na mwalimu wao wa darasa wanahitaji uniti 50 za damu.
“Tayari wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Alfred Rulenge inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge wamechangia uniti 46 za damu kusaidia wenzao,” amesema.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo leo Alhamisi Novemba 9,2017 asubuhi, Dk Ndyekobora amesema timu ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera imewasili Ngara kusaidiana na wenzao kuwafanyia uchunguzi na kuwatibu majeruhi hao.
“Watakaobainika kuhitaji huduma maalumu watahamishiwa hospitali zingine kulingana na taarifa ya madaktari,” amesema Dk Ndyekobora.
Mbali ya damu, majeruhi pia wanahitaji mashuka na mablanketi zaidi ya 50 kutokana na yaliyopo kutotosheleza mahitaji.
Amesema baadhi wamelazimika kulala sakafuni kutokana na vitanda kujaa.
“Msaada wa chakula pia unahitajika kwa ajili ya majeruhi hawa ambao wametoka maeneo ya mbali kiasi cha kutowezesha wazazi, ndugu, jamaa na marafiki kuwaletea chakula,” amesema Dk Ndyekobora.
Usafiri kwa ajili ya kuwahamishia hospitali zingine pia ni miongoni mwa mahitaji ya dharura yanayohitajika kuokoa maisha ya majeruhi hao.
Amesema baadhi wamebainika kuwa na vipande vya vyuma vilivyotokana na mlipuko wa bomu uliotokea jana Jumatano Novemba 8,2017 wakati wanafunzi hao wa darasa la kwanza wakiingia darasani.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Aidan Bahama amepiga marufuku biashara ya vyuma chakavu katika maeneo ya shule akionya kuchukua hatua dhidi ya mwalimu mkuu na wakuu wa shule watakaobainika kuruhusu biashara hiyo.
Amri ya Bahama imetokana na uchunguzi wa awali wa polisi kubaini mwanafunzi mmoja aliokota bomu na kulihifadhi kwenye begi lake kwa lengo la kuliuza kama chuma chakavu.
Halmashauri kugharamia mazishi
Bahama amesema halmashauri imechukua dhamana ya kugharimia majeneza na shughuli za mazishi ya watoto watano waliokufa katika tukio hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Erick Nkilamachumu na mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Ngara, George Lubagola wameiomba Serikali kuimarisha ulinzi na ukaguzi kwa watu wanaingia nchini kutoka Burundi ili kudhibiti uingiaji holela wa silaha na mabomu ya kutupa kwa mkono.
Kijiji cha Kihinga ni miongoni mwa maeneo yanayopakana na nchi jirani za Burundi na Rwanda na kuna mwingiliano wa watu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
No comments:
Post a Comment