Uamuzi wa Mahakama Kuu ulitolewa Novemba 10,2017 katika Kanda ya Dar es Salaam umeizuia CUF kujadili na kuwafukuza uanachama wabunge hao na madiwani wawili wa viti maalumu.
Hata hivyo, Mahakama ilitoa uamuzi huo huku tayari chama hicho kikiwa kimeshawavua uanachama na baadaye kupoteza nafasi zao za ubunge.
Wabunge hao ni Miza Bakari Haji, Saverina Mwijage, Salma Mwasa, Raisa Mussa, Riziki Mngwali, Hadija Salum Al-Qassmy, Saumu Sakala na Halima Mohamed.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Novemba 30,2017, Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai amesema shauri lililofunguliwa ni kupinga uamuzi wa CUF kuwafukuza uanachama na kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama bado uamuzi wa mwisho haujatolewa.
"Uamuzi uliotolewa na Mahakama ni wa awali kuhusu pingamizi na uliwalenga walalamikiwa ambao ni baraza la wadhamini wa CUF na uongozi wake ambao uliamuru walalamikiwa wasitishe utekelezaji wa uamuzi wa kuwafukuza uanachama na vilevile, kutojadili suala lolote kuhusu uanachama wa walalamikaji hao hadi Mahakama itakapokamilisha shauri la msingi," amesema.
Amesema ifahamike vyema kuwa hakuna sehemu yoyote katika uamuzi huo wa Mahakama inapoelekezwa wabunge hao wanatakiwa kurudishiwa ubunge.
Kagaigai amesema kumekuwapo tafsiri isiyo sahihi ya uamuzi huo wa Mahakama inayotolewa na baadhi ya watu na vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya jamii kusambaza taarifa potofu kuwa wabunge hao wamerejeshwa bungeni kwa uamuzi huo wa Mahakama baada ya kurejeshewa uanachama wa CUF.
Amesema wabunge hao waliiandikia ofisi ya Bunge barua wakiomba kufahamishwa utaratibu utakaotumika kuwarejesha bungeni.
"Tunapenda umma uelewe kwamba, nafasi za ubunge zilizoachwa wazi baada wabunge husika kufukuzwa uanachama zilijazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa sheria na wabunge waliopatikana kujaza nafasi hizo wanaendelea kutekeleza majukumu yao ya kibunge ipasavyo," amesema.
No comments:
Post a Comment