Monday, October 16

WAZEE WA BARAZA WAKWAMISHA KESI YA BILIONEA MSUYA

Kesi ya mauaji ya mfanyabiahara wa madini, Bilionea Erasto Msuya iliyokuwa iendelee kusikilizwa leo katika Mahakama kuu kanda ya Moshi, imelazimika kuahirishwa hadi Oktoba 18, mwaka huu kutokana na kukosekana kwa wazee wa baraza la mahakama hiyo.
Kesi hiyo ambayo inasikilizwa na Jaji Salma Maghimbi, imepangwa kusikilizwa kwa kipindi cha mwezi mmoja mfululizo katika mahakama hiyo, ambapo upande wa jamhuri utaendelea kutoa ushahidi.
Kwa mujibu wa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu kanda ya Moshi, Benard Mpepo kesi hiyo imelazimika kuahirishwa kutokana na mmoja wa wazee wa baraza kukosekana mahakamani.
Alisema kesi hiyo ambayo ilikuwa na wazee wa baraza watatu, mmoja ambaye ni Zacharia Nato alifariki miezi miwili iliyopita na kubaki wazee wawili ambapo kwa mujibu wa sheri walionekana kukidhi matakwa ya kuendelea kusikiliza kesi hiyo lakini mzee moja kati ya wawili waliobaki hakuweza kufika mahakamani kutokana na matatizo ya kifamilia.
Katika kesi hiyo shahidi wa tisa Inspekta wa Polisi Samweli Maimu, upande wa jamhuri ambaye alikuwa aendelee kutoa ushahidi wake leo ambapo sasa atalazimika kuendelea Oktoba 18.
Bilionea msuya aliuawa kwa kupigwa risasi Agosti 7, mwaka 2013 eneo la Mjohoroni wilayani Hai ambapo washtakiwa saba wanatuhumiwa kuhusika na mauaji hayo.

No comments:

Post a Comment