Thursday, October 12

Wakili wa Scorpion asababisha kesi kuahirishwa


Dar es Salaam. Kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi inayomkabili Salum Njwete (34) maarufu Scorpion, imekwama kusikilizwa kutokana na wakili wake kutokuwepo mahakamani.
Kesi imekwama kusikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kutokana na wakili Juma Nassoro anayemwakilisha Njwete kuwa Mahakama Kuu katika shauri lingine.
Wakili wa Serikali Nassoro Katuga mbele ya Hakimu Mkazi, Flora Haule alieleza shauri lilipangwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi lakini wakili wa mshtakiwa alikuwa Mahakama Kuu.
Katuga alisema kwa kuwa mshtakiwa ana haki kisheria ya kuwakilishwa wamekubaliana na wakili wake kesi iendelee kesho Ijumaa.
Hakimu Haule alikubali ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi leo kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.
Katika hati ya mashtaka, Njwete anadaiwa Septemba 6 mwaka jana Buguruni Sheli wilayani Ilala alimjeruhi Said Mrisho. Pia, anadaiwa kumwibia mali yenye thamani ya Sh476,000.
Mshtakiwa anadaiwa alimjeruhi Mrisho kwa kumchoma kisu machoni, mabegani na tumboni ili kujipatia mali bila kikwazo.

No comments:

Post a Comment